Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema serikali kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuyaendeleza, kukarabati na kutunza kumbukumbu zote za kihisitoria zilizoachwa na wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini katika eneo la Kampasi ya Solomon Mahlangu.
Mhe. Gekul ameyasema Januari 18, 2022 mjini Morogoro wakati alipotembelea makaburi 97 ya wapigania uhuru wa chama cha ANC cha Afrika ya Kusini yaliyoko Kampasi ya Solomon Mahlangu na yanatunzwa na SUA kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo amesema mali kale na kumbukumbu zote za kihisitoria zinapaswa kutunzwa vizuri ili vizazi vya sasa na baadae viweze kutambua historia za nchi zao.
“Tutayatangaza tukishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii yawe ni maeneo ya vivutio ya kiutalii wa kihistoria kwa wenzetu ambao wanapenda kupata historia za nchi zao, lakini pia na watalii wengine wafike kwenye maeneo haya kwa hiyo tuko hapa kwa ajili ya kazi hiyo na lengo ni kushirikiana na hizo nchi kwa ukaribu ili tuone na wao wanashirikije katika kutunza historia hii” amesema Gekul
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akisikiliza maelezo kutoka kwa Bw. Ali Mkopi mtumishi wa SUA anayelijua vizuri eneo hilo la Makaburi ya Wapigania Uhuru wa ANC
Aidha ameongeza kuwa kwa sasa Wizara kwa kushirikiana na SUA kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika inapaswa kutambua watoto na mama wa familia za wapigania uhuru wa Afrika ya Kusini ili nao wawe sehemu ya historia pale zinapokuja familia zao kutoka Nchi ya Afrika ya Kusini.
Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Bw. Boniface Kadili amesema eneo la Mazimbu ni sehemu moja wapo ya Ukombozi wa Bara la Afrika na jitihada zilizopo kwa sasa kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ni kulitangaza katika gazeti la Serikali ili eneo hilo liweze kuwa katika Ulithi wa Taifa.
“Eneo hili likishalindwa kisheria sio kwamba linakuwa ni miliki ya Maliasili au Wizara yetu bado litaendelea kuwa miliki ya SUA ila sisi tunachofanya ni kutoa ushauri wa kitaalamu wa kuhifadhi eneo ili muhimu. Amesema Boniface Kadili Mratibu wa Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika “ amesema Gekul
Aidha Mhe. Gekul ameagiza Afisa Utamaduni Mkoa wa Morogoro na Afisa Utamaduni Manispaa ya Morogoro kuhakikisha wanatambua maeneo yote ya kihistoria ya asili ndani ya maneo yao ili kumbukumbu hizo zitumike kwenye historia ya Tanzania.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando amesema katika wilaya ya Morogoro yapo maeneo mengi ya kihistoria ya asili ambayo yanapaswa kutunzwa lakini changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni ukosefu wa watu ambao wanaweza kutunza maeneo hayo hasa yanayohusu Machifu waliofia katika wilaya ya Morogoro.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando (aliyevaa suti)
Akitoa taarifa ya namna ambayo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kilivyopewa majengo na maeneo hayo ya Kampasi ya Solomon Mahlangu kutoka kwa wapigania Uhuru wa Afrika ya Kusini Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi, Dkt. Geoffrey Karugila amesema kambi hiyo ilianzishwa mwaka 1978 lengo likiwa ni kupigania uhuru wa Nchi ya Afrika ya kusini kupitia Chama cha ANC.
Dkt. Geoffrey Karugila ameendelea na kusema mwaka 1999 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikabidhi eneo hilo rasmi kwa SUA ambapo mwezi Machi mwaka 1999 Baraza la Chuo liliamua kubadilisha jina kutoka SUMAFUCO na kuliita Kampasi ya Solomon Mahlangu na lina miundombinu mbalimbali iliyoachwa ikiwemo Madarasa, Hospitali na Jengo la Utawala.