Tafiti zimeonesha kuwa, kwa mwaka mmoja Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi bilioni 19 kutokana na athari zinazotokana na Minyoo tegu ya Nguruwe kwa jamii ikiwemo matibabu na kutupa nyama yenye maambukizi
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi CYSTINET Africa Prof. Helena Ngowi kwenye Warsha ya kujadili mrejesho wa matokeo ya Utafiti kuhusu namna ya kudhibiti Mnyoo Tegu ya Nguruwe Tanzania iliyofanyika Jijini Dodoma.
“Ukiangalia hapa nchini Tanzania wagonjwa wa kifafa takribani 212 ya wagonjwa wote wa ugonjwa huo utakuta wanatokana na Minyoo tegu ya Nguruwe na kuigharimu jamii shilingi bilioni 12 kwaajili ya matibabu na hasara ya shilingi bilioni 7 kutokana na kutupwa kwa nyama ya nguruwe nyenye maambukizi, alifafanua Prof. Helena.
Aidha Prof. Helena amesema pamoja na magonjwa yanayosababishwa na tegu wa Nguruwe (Taenia solium) kuwa na athari kiuchumi,kiafya na kijamii kwa waathirika na familia zao lakini hayajapewa kipaumbele nchini Tanzania.Mkurugenzi wa Mtandao wa Kisayansi CYSTINET Africa Prof. Helena Ngowi akiwasilisha matokeo ya utafiti kwenye warsha hiyo jijini Dodoma.
Mkurugenzi huyo wa CYSTINET Afrika amesema kimataifa,kwa mujibu wa ripoti yam waka 2014 ya Shirika la Chakula duniani FAO na Shirika la afya Duniani WHO mnyoo tegu wa nguruwe ni tishio namba moja kati ya magonjwa ya vimelea kundi hili yanayoenezwa kwa njia ya chakula.
“Muhtasari huu wa matokeo umetokana na uchambuzi wa kina wa matokeo ya tafiti yaliyochapishwa katika kipindi cha miaka 26 hadi kufikia Disemba 2021 Tafiti hizi zilifadhiliwa na wafadhili mbalimbali, ikiwemo Serikali ya Tanzania (hasa kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi)” alieleza Prof. Ngowi.
Hata hivyo amesema Tafiti zaidi zinahitajika kubaini ukubwa wa tatizo na kutafuta suluhisho endelevu ingawa tayari katika kipindi cha mwaka 1995 -2021 zimefanyika tafiti zaidi ya 78 zikiwemo zilizohusu kiwango cha mambukizi kwa binadamu, kiwango cha maambukizi kwa nguruwe, mgongano wa magonjwa mengine, vichocheo vya maambukizi, madhara ya kiuchumi, kudhibiti maambukizi kwa binadamu, kudhibiti maambukizi kwa nguruwe, Mikakati ya elimu kwa jamii pamoja na Nyanja zingine ndogo ndogo,
Prof. Helena amesema tafiti nyingi zinaonesha zililenga kuangalia maambukizi kwa nguruwe na matokeo mengi ya tafiti hizo yameonesha maambukizi kwa nguruwe waliopo vijijini waliochunguzwa kwa kukagua kwenye ulimi maambukizi ni asilimia 6.0% – 17.4% na kwa kipimo cha Ag-ELISA ni 1.5% – 33.3%.
Amesema matokeo ya utafiti ya Mnyoo kamili tumboni kwa binadamu (taeniasis) kwa kipimo cha Coproantigen ELISA ilionesha ni 2.3% – 5.2%, utafiti wa vimelea mwilini mwa binadamu (cysticercosis) kwa kipimo cha Antigen ELISA imeonesha ni 16.7%, Vimelea kwenye ubongo wa binadamu (neurocysticercosis) vipo kwa wagonjwa wa kifafa zaidi wakati Vimelea kwenye nyama ya nguruwe kwa ukaguzi wa kaiwaida wamebaini ni asilimia 0% - 18.2%.
Mtafiti huyo kutoka SUA amesema vichocheo vikubwa vya maambukizi hayo ya Minyoo tegu ya nguruwe ni Ufugaji wa nguruwe wa kienyeji wa kuacha kuzagaa mitaani kujitafutia chakula lakini pia kutokuwepo kwa vyoo kwenye maeneo yanayofuiga nguruwe kwa wingi hasa vijijini bila kusahau kutopika nyama hiyo vizuri.
Kwa upande wake Dkt. Benard James Ngowi ambaye ni Mtafiti na Mhadiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam kutoka Ndaki ya afya na sayansi shirikishi kampasi ya Mbeya na Mtafiti mwandamizi katika taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu kituo cha NIMR Muhimbili amesema matokeo yanaonekana kwa binadamu katika hali mbili ambapo ya kwanza ni ile ya binadamu anakuwa na mnyoo kamili kwenye utumbo na ya pili ni ile hatua ya lava kwenye misuli na ubongo.
“Mtu anapokuwa na lava hao kwenye misuli wanakuwa kama mchelemchele yani vitu vyeupe vyeupe kwenye nyama na vikiwa kwenye Ubongo wa ndio vinasababisha mtu kupata kifafa lakini wakiwa minyoo tuu kwenye utumbo wanasababisha mtu kupata dalili zisizo za maalumu kwa ugonjwa huo kama vile kupoteza hamu ya kula,tumbo kutokuwa vizuri kujisikia kuharisha lakini haarishi yani ni kama dalili za mtu mwingine mwenye minyoo ya kawaida” alifafanua Dkt. Ngowi.
Dkt. Benard James Ngowi ambaye ni Mtafiti na Mhadiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam kutoka Ndaki ya afya na sayansi shirikishi kampasi ya Mbeya na Mtafiti mwandamizi katika taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu kituo cha NIMR Muhimbili akifafanua jambo kwa Wandishi wa habari.
Amesema takwimu nyingi ni zile za mnyoo ambaye anakuwa nje ya utumbo kama vile kwenye Ubongo, Misuli, Moyo na chini ya ngozi ambapo minyoo hukaa huko lakini kubwa zaidi takwimu zenyewe zinatofautiana tofautiana kati ya Wilaya na Wilaya kulingana na namna jamii inavyofuga nguruwe hao kwa kuacha watembee mitaani au kufugia ndani ambapo kwenye takwimu kubwa ni Mbozi ambapo imefikia hadi asilimia 30%, Iringa 16.7% ya maambukizi huku Kinondoni Jijini Dar es salaamu kwa wanaohudhuria kliniki ya Kifafa asilimia 8% imesababishwa na uwepo wa Minyoo tegu kwenye Ubongo.
Aidha Dkt. Ngowi katika kumaliza tatizo hilo amehimiza kufuatwa kwa mapendekezo yote ya utafiti huo ambayo yamehimiza kukomesha ufugaji wa nguruwe na kuacha wajitafutie chakula mitaani na kuwa na machinjio maalumu ya nguruwe ili nyama iweze kukaguliwa kabla ya kwenda kuuzwa na kuchomwa.
Mradi wa CYSTINET Africa umefadhiliwa na Wizara ya Elimu na Utafiti ya Serikali ya Ujerumani (BMBF) ambao umeratibiwa na SUA, Mtandao huu unajumuisha Taasisi 5 katika Nchi Nne za washiriki ambazo ni SUA, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania, Chuo Kikuu cha Zambia Pamoja na Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane - Msumbiji.
Wadau wa warsha hiyo wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo ya utafiti kuhusu minyoo tegu ya Nguruwe nchini.
NA: CALVIN GWABARA - DODOMA