Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia Mhe. Nape Moses Nnauye ameupongeza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuanzisha Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi kikakati ili kuinua Elimu na Jamii ya Mikoa inayozalisha asali na mazao ya chakula kwa wingi.
Kauli hiyo ameitoa tarehe Januari 9, 2023 alipotembelea Kampasi hiyo iliyopo katika Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano na mtandao kwenye Kampasi hiyo na Wilaya hiyo kwa ujumla.
“Nimefurahishwa na namna ambavyo Kampasi hii ya SUA Mizengo Pinda mmetengeneza kimkakati sana kwamba kwa mazingira ya huku na kwa sababu sasa Mfalme wa Nyuki yupo hapa basi mambo yanakwenda Kinyuki, Kiutalii, Uwindaji, Kilimo na kadhalika hili jambo ni zuri sana na mimi nadhani tuone namna ya kuhamasishana na wengine wafanye kama nyinyi” amefafanua Mhe. Nape.
Ameongeza “Kuna Mbunge fulani maarufu sana pale Bungeni anaitwa Mhe. Kishimba, hajasoma lakini ana hoja nzito sana siku moja alituuliza hivi nyinyi nani aliwaambia mwanangu lazima asome miaka saba shule ya msingi? halafu anaenda Sekondari halafu mnampeleka Chuo Kikuu, mnamchukua ana miaka saba mnamrudisha ana miaka 23 halafu mnaniambia nimtafutie ajira sasa nyinyi wasomi vipi? Ukiangalia hoja yake ni ya msingi sana” amesema Mhe. Nape
Aidha Mhe. Nape amesema inaonekana watoto wanabebeshwa mambo mengi sana na hadi kufikia kumaliza wanakuwa wamechoka na hata uwezo wa kufanya kazi hawana, hivyo hilo ambalo limefanywa na SUA kupitia kampasi yake ya Mizengo Pinda limemfurahisha sana.
Amewataka wasomi kufikiria namna ya kumsaidia mtu kumudu mazingira yake kama ilivyo maana ya Elimu yenyewe na kwamba hata yeye huwa anafikiria mambo mengi magumu aliyosoma ambayo hajawahi kuyatumia mahali popote pale kwenye maisha yake kwa hiyo wakati huu ambapo mitala inapitiwa upya waone sababu ya kupunguza mizigo kwa wanafunzi.
Awali akitoa taarifa fupi ya kuanzishwa kwa Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo mwaka 2019 Rasi wa ndaki hiyo Prof. Josiah Katani amesema ni kupanua wigo wa SUA kitaaluma na kitafiti katika nyanja za Kilimo, Mifugo, Ufugaji Nyuki na Utalii hususani katika mikoa ya Nyanda za juu kusini.
“Kampasi hii ilianza kudahili wanafunzi katika mwaka wa masomo wa 2020 -2021 katika kozi tatu ambazo ni Shahada ya Sayansi za Usimamizi wa Rasilimali Nyuki, Stashahada ya Kilimo Usimamizi na Uzalishaji wa Mazao pamoja na Astashahada ya Utalii na Uwindaji” ameleza Prof. Katani.
Rasi wa Ndaki ya SUA Kampasi ya Mizengo Pinda Prof. Josiah Katani akitoa taarifa fupi na malengo ya kuanzishwa kwa kampasi hiyo Mkoani Katavi.
Aidha amefafanua kuwa uanzishwaji wa kozi hizo ni wa kimkakati kutokana na mazingira ya eneo hilo kwani ni mazingira ya kilimo, kuwa na makundi makubwa ya nyuki na uhimizwaji wa ufugaji wake kuwapatia wananchi kipato lakini pia ni eneo la utalii kutokana na kuwa na Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo ni moja ya hifadhi kubwa nchini.
Wanajumuiya ya SUA,Wananchi na viongozi mbalimbali wa Wilaya na walioambatana na Mhe. Waziri wakifuatilia mkutano huo.