Katika kuhakikisha wakulima wanakabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia mradi wa FOODLAND waliandaa na kutoa mafunzo ya namna ya kutumia Matandazo katika Kilimo hususan kwa wakulima wa zao la Maharage kutoka Kijiji cha Ndole Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo ambayo yalifanyika mwezi Julai, Mratibu wa Mradi wa FOODLAND, Prof Suzan Msolla ameeleza kuwa matandazo hayo yanasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia unyevu wa maji ardhini, kuzuia kuota kwa magugu na joto kutokuwa jingi kwenye udongo ambapo katika utafiti unaoendelea kufanyika tayari wakulima wameona ubora wa kila aina ya tandazo.
“Moja kati ya tandazo ambalo tumelionyesha ni tandazo la aina kama ya plastiki kutoka kiwandani ambalo likikaa mwaka mmoja shambani linaoza, tumetumia tandazo hili ili tuweze kuona ubora wake na ubora wa yale matandazo ya asili hivyo tumewaleta wakulima ili wao wenyewe waweze kuangalia na kutoa maamuzi ya aina gani ya matandazo wanaweza wakayatumia na hii ni baada ya wao kufanya tathimini kuona namna wanaweza kuyapata”, alisema Prof Msolla.
Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia Dkt Boniface Masawe akionyesha kwa wakulima utofauti wa ubora wa matandazo
Miongoni mwa wakulima waliopatiwa mafunzo hayo walielezea uzoefu wao ambapo ndugu Daudi Tesha yeye alieleza kuwa pamoja na kugundua kuwa matandazo yanaongeza mavuno, wakati mwingine imewalazimu kulima zao la Maharage pasipo kutumia Matandazo na hiyo ni kutokana na changamoto ya upatikanaji wa Matandazo hayo.
“Kule kijijini sehemu ambayo tunalima kwa matandazo, majani yanakuwa si mengi kama kule ambako tunalima bila matandazo. Nimefurahi leo nimepata mbinu mpya ya kukabiliana na uhaba wa matandazo, kwamba naweza kutumia matandazo ya kiwandani na yakanisaidia katika kilimo hivyo niombe tu elimu hii iweze kuwafikia na Wakulima wengine wa vijijini ambao hawakupata fursa ya kuwa hapa leo ili na wao wakanufaike”, alieleza Bwana Tesha
Kwa upande wake, Estelia Venas amesema kuwa katika mafunzo hayo amejifunza njia mpya kabisa ambazo alikuwa hazifahamu hivyo matarajio yake mara baada ya kutumia njia hiyo mpya ya matandazo ya kiwandani anategemea kupata mavuno zaidi yatakayokwenda kumkomboa kiuchumi.
Mkulima mwingine aliyefahamika kwa Jina la Kimweri Julius ambaye ni mara ya pili kupata mafunzo kutoka SUA ameeleza kuwa awali walikuwa wakilima na kupanda mazao pasipo kuzingatia umbali wa shimo kwa shimo, akapata elimu ya namna sahihi ya upandaji na ameona matunda mazuri ya kufuata njia hiyo.
“Lakini kwa sasa changamoto iliyopo ni majani ambayo yanakuwa mengi sana shambani na suluhisho ndo hilo nimefundishwa leo hivyo nakwenda kulifanyia kazi ili nami niweze kupata manufaa yale niliyoyaona
katika shamba darasa”, alisema Julius.
Imeandikwa na Amina Hezron na Calvin Gwabara – SUAMEDIA