Hafla ya futari kwa wafanyakazi na wanafunzi wa SUA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martini Shigella amempongeza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda  kwa kuandaa hafla ya futari kwa ajili ya jumuiya ya chuo pamoja na wanazuoni kwani itazidi kuongeza umoja, upendo na mshikamano miongoni mwao.

SUA

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Martini Shigela akitoa pongezi kwa SUA

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Shigella amesema hafla hiyo iwe fundisho kwa taasisi zingine ambazo hazijawahi kufanya jambo kama hilo ili likaongeze mshikamano katika kazi zao.

“Nawashukuru sana Prof. Chibunda na wafanyakazi pamoja na wanazuoni wa SUA kwa kuonyesha upendo  Mwenyezi Mungu akawafanyie heri katika mambo yenu na pale mlipotoa basi akapajazie pakaongezeke zaidi”, alisema Mhe. Shigela.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  Prof. Raphael Chibunda akiwakaribisha wageni waalikwa kwenye futari

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema nia ya kuandaa futari hiyo ni kuhakikisha chuo kinazidi kudumisha mshikamono uliopo baina ya Manejimenti, wafanyakazi na wanafunzi wake.

Amewataka kuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu katika kipindi kizima cha kumalizia mfungo wa Mwezi wa Ramadhani ili azidi kuwaongezea nguvu upendo na mshikamano miongoni mwao na majirani wanaokizunguka chuo hicho.

Sheikh Selemani Lukanda akiwasilisha salamu za Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Morogoro

Kwa upande wake mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Sheikh. Selemani Lukanda amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kuona haja ya kuandaa hafla hiyo ya kuonyesha umoja na udugu ambao uliasisiwa na wazee wa zamani ambao walikwisha tangulia mbele za haki kwa kuwa pesa zilizotumika kuandaa hafla hiyo zingeweza kutumika kufanya majukumu mengine ya chuo.

“Hii ndiyo tunu ambayo nchi yetu ya Tanzania imetunukiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa mambo kama haya ni nadra sana kuyaona katika nchi zingine kuwaona waislamu wanajumuika na wasiowaislamu kupata futari kwa pamoja katika hali ya usalama na amani kabisa, hivyo ni muhimu kuzidi kumuomba Mungu aendelee kutulinda na kutusimamia amani hii iendelee kuwepo “, alisema Sheikh Lukanda.











Habari na Picha: Amina Hezron - SUAMEDIA

 

Share this page