Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilianzishwa rasmi mnamo tarehe 01 Julai 1984 kwa Sheria ya Bunge Na. 6 ya mwaka 1984. SUA ilipewa Hati Idhini mwaka 2007 chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu Na. 7 ya mwaka 2005. Chuo hiki kinatoa wataalamu kuanzia ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada za Kwanza, Shahada za Umahiri na Shahada za Uzamivu.Watalaamu wanaotolewa na SUA hutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa kupitia huduma yao katika sekta mbalimbali serikalini na zile za kibinafsi.
Chuo kimejiwekea malengo ya kimkakati ambayo ni kuongeza udahili wa wanafunzi, miradi ya utafiti na kuboresha huduma za ugani na ushauri wa kitaalamu. Hata hivyo kwa miaka mingi Chuo kilishindwa kufikia malengo hayo kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo uchakavu wa miundombinu na mifumo ya huduma za jamii.
Kupitia Serikali ya Awamu ya Tano, Chuo kimetatua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na
- Kujenga Maabara Mtambuka Kampasi Kuu,
- Maabara ya Sayansi Solomon Mahlangu,
- Kukarabati viwanja vya michezo,
- Kuanzisha shamba la mafunzo la mfano,
- Kukarabati Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama,
- Kukarabati madarasa na mabweni,
- Kununua mabasi, pamoja na
- Kupanua na kusajili Hospitali ya SUA.
Maboresho hayo ya miundombinu yamekifanya Chuo kuongeza programu mpya za masomo 26, kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 9,165 mwaka wa masomo 2015/16 hadi 13,199 mwaka wa masomo
2019/20. Katika kipindi hiki jumla ya wataalamu 13,178 ambao wamehitimu katika program mbalimbali.
Menejimenti ya Chuo inatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Profesa Raphael T. Chibunda
Makamu Mkuu wa Chuo