Waganga wa tiba asili waaswa kutochanganya dawa za asili na za kisasa

Waganga na wazalishaji wa dawa za asili na mitishamba nchini Tanzania wameshauriwa kuendelea kuzingatia ubora wa bidhaa zao na kuepukana kabisa na tabia ya kuchanganya  dawa za asili na zile za  kisasa ili kupunguza athari zinazoweza kuwapata watumiaji.

GRILI Project SUA

Picha ya pamoja ya wajumbe wa mkutano mkuu wa maradi wa GRILI

Wito huo umetolewa na kiongozi wa mradi wa utafiti unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wa kuongeza ubunifu katika mimea dawa ili kuboresha Maisha (GRILI) Dkt. Faith Mabiki wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa mradi huo uliofanyika Mkoani Njombe hivi karibuni.

“Katika wakati huu ambao Serikali inahimiza dawa asili zilizosajiliwa zipatikane katika maduka ya dawa za kisasa na uwepo wa maduka ya dawa za asili kwenye hospitali na maeneo mbalimbali kwa wingi nchini ni lazima sasa dawa hizo ziweze kuwa halisi na kufikia viwango vinavyotakiwa na wataalamu wetu wa tiba asili kutofanya udanganyifu kwa wateja ili waweze kuaminika na kutoathiri afya za watu” alisema Dkt. Mabiki

Dr, Mabiki amesema lengo la wao kufanya tafiti hizo ni kuhakikisha dawa za asili nchini zinakuwa bora na zifikie viwango vya kimataifa na kuweza kusafirishwa kwenda kuuzwa kwenye nchi zingine duniani ili kushika soko la dawa za asili linalokua kwa kasi duniani kwa sasa.

Dk. Mabiki alitahadharisha kuwa kufanya udanganyifu kutasababisha kuharibu sifa na soko la dawa za asili kutoka Tanzania kwenye soko la kimataifa. Hivyo ameiomba serikali kupitia mamlaka zake za uhamasishaji, uratibu, usimamizi, uendelezaji na udhibiti wa dawa asili nchini kuhakikisha watengenezaji wa dawa asili hawachanganyi  dawa za asili na zile za  kisasa ili kupunguza athari zinazoweza kutokea kwa watumiaji.

Amesema mara baada ya kukamilika kwa tafiti mbalimbali za mimea dawa na dawa za asili  zinazofanywa na wanafunzi wa shahada za uzamivu na uzamili kupitia mradi huo wa GRILI, wataziwasilisha serikalini kwenye mamlaka husika ili kuweza kuona matokeo hayo ya kisayansi yatakayopatikana ili yawawezeshe kuchukua hatua na kufanya maamuzi sahihi yanayotokana na sayansi.

Mtafiti mkuu wa mradi wa GRILI Dkt Faith Mabiki akichangia jambo kwenye mkutano mara baada ya wasilisho la wanafunzi

Kwa upande wake, Dkt. Doreen Ndosi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amesema katika wakati huu ambao dunia inakabiliana na changamoto ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kisasa ni lazima suala la udanganyifu kwa baadhi ya waganga wa tiba asili uliobainika wa kuchakachua dawa za asili na za kisasa utafutiwe ufumbuzi maana unachangia katika tatizo hilo.

“Usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni changamoto kubwa duniani kwa sasa na kitendo cha dawa za asili kuchanganywa na dawa za kisasa kunaweza kuchangia sana katika kuongeza tatizo hilo hivyo mamlaka husika zina kila sababu ya kulivalia njuga swala hili na kulikomesha kwa maslahi mapana ya watumiaji wa dawa hizo za asili” alisisitiza Dkt. Ndosi

Akichangia kuhusu changamoto hiyo ya udanganyifu wa baadhi ya waganga wa tiba asili wanaochanganya dawa za asili na za kisasa, kiongozi wa upimaji wa dawa asili dhidi ya virusi katika Mradi wa GRILI ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuendeleza Viwanda Tanzania (TIRDO), Prof. Madundo Mtambo amependekeza tafiti zaidi zifanyike ili kuisaidia Serikali kupata Ushahidi wa kutosha ili kufanya maamuzi sahihi katika suala hili muhimu linalogusa afya za binadamu na Wanyama.

Katika mkutano huo mkuu wa mwaka wa mradi wa GRILI ambao umefanyika mkoani Njombe, wanafunzi wote sita wanaofanya tafiti katika maeneo mbalimbali ya mimea dawa na dawa asili zinazotumika nchini walipata nafasi ya kuwasilisha maendeleo ya tafiti zao mbele ya wadau na wasimamizi wa tafiti zao na kisha kupata mapendekezo na michango muhimu ya kitaaluma ya namna ya kuboresha tafiti zao kama sehemu ya kukamilisha matakwa ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine katika shahada zao.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wadau wengine wa mradi wa GRILI kutoka nchi mbalimbali duniani kwa njia ya mtandao (ZOOM) na walishiriki kikamilifu katika kuwasilisha mawazo na michango yao ili kufikia malengo makubwa ya mradi huo kwa taifa.


Wajumbe wakifatilia mawasilisho ya tafiti za wanafunzi katika mkutano 

Share this page