Wadau wa Kilimo wahimizwa kuwekeza kwenye zao la Kahawa

Sekta binafsi na za umma zimeshauriwa kuongeza uwekezaji kwenye zao la Kahawa kutokana na umuhimu wa zao hilo na fursa za kiuchumi kwenye maeneo ya kilimo cha kahawa nchini.

SUA

Kiongozi wa Mradi wa TRADE HUB Prof. Reuben Kadigi akizungumza na wadau kuhusiana na malengo ya mradi katika warsha ya kuwasilisha matokeo ya utafiti

Hayo yamesemwa mnamo tarehe 1 Juni 2022 na mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Joseph Rajabu Kangile alipokuwa akiwasilisha matokeo ya utafiti wa awali juu ya kutambua faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira zitokanazo na biashara ya kahawa Tanzania, Jijini Dodoma. Utafiti huo ulilenga kuongeza uelewa kwa ajili ya kuchangia katika uundaji wa sera zitakazochochea biashara ya kahawa inayolimwa kwa uendelevu, usawa wa kijamii na uendelevu wa jumla katika mnyororo wa usambazaji Kahawa.

“Pamoja na kuwa kuna changamoto nyingi ambazo tunatakiwa kuendelea kuzitatua lakini kimsingi ni kwamba tunatakiwa tuhakikishe tunawekeza kwenye kahawa kwenye maeneo yanayofaa kwa kilimo cha kahawa, kwasababu mapato yanayopatikana kwenye biashara ya Kahawa yana mchango zaidi kwenye kaya maskini kuliko ukiwekeza kwenye kitu au fursa nyingine” alisema Kangile.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Joseph Rajabu Kangile akiwasilisha matokeo ya utafiti

Kangile ameeleza kuwa matokeo ya utafiti wa awali yanaonyesha kwamba uwekezaji wa ndani kwenye masoko na uidhinishaji (certifications) kuwafikia wadau bado ni mdogo na kwamba watu wengi hawajafikiwa na huduma za uidhinishaji sambamba na uwepo wa changamoto ya kuenea kwa magonjwa ya Kahawa kama vile CBD yanayokwamisha juhudi hizo.

“Vilevile kuna upungufu wa biashara na upatikanaji wa baadhi ya pembejeo zinazotakiwa katika kilimo endelevu cha kahawa mfano dawa asilia (hasa kwa kilimo hai), kutopatikana kwa urahisi wa faida ya bei na faida ya mavuno inayotarajiwa kutokana na kujiunga na mipango ya uidhinishaji pamoja na gharama kubwa za uidhinishaji na ukaguzi” alisema Kangile.

Hivyo amewataka wakulima kukaa kwenye vikundi ili iwe rahisi kwa wao kupata huduma pasipo changamoto kubwa.

“Kimsingi kwa sasa kwa hali jinsi ilivyo mifumo ya uidhinishaji inafaida kubwa zaidi kwenye mazingira lakini ina faida kidogo kwa mtu mmoja mmoja hasa kwa wale wakulima ambao ushiriki wao kwenye vikundi ni mdogo hivyo wakulima na wadau wengine waweze kuelimishwa ili kuutambua uidhinishaji kama fursa ya kuongeza masoko ya nje”, alisema Kangile.

Akizungumzia kuhusiana na lengo la utafiti huo, Mkuu wa Mradi wa TRADE HUB Prof. Reuben Kadigi amesema kuwa wao kama watafiti wameona ni muhimu kuyapa kipaumbele katika mradi mazao ambayo yanachangamoto ya kibiashara hapa nchini. 

“Zao la kahawa zamani lilikuwa zao tegemezi la kibiashara ambalo watu waliliona linasaidia lakini baadae kidogo tukaona limeporomoka lakini kuporomoka huku inasababishwa na changamoto za kisera na kibiashara hasa bei”, alisema Prof. Kadigi.

Wadau na watafiti wakifatilia maelezo ya wasilisho

Mradi Wa TRADE HUB unafanya utafiti kwenye mazao mbalimbali ya kibiashara ikiwemo kahawa, sukari, soya na wanyamapori ambayo yalikuwa na mchango mkubwa katika kuinua Maisha ya jamii na Taifa kwa kupata fedha za kigeni. Mradi unasaidia kubainisha changamoto za kuzorota kibiashara kwa mazao hayo na kutafuta ufumbuzi ili kuongeza faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira zitokanazo na biashara za mazao hayo.

Imeandikwa na: Amina Hezron - SUAMEDIA
 

Share this page