Utafiti wa mbegu za mpunga zinazostahimili mabadiliko ya tabia nchi

Licha ya Mradi wa CLIMATE-SMART AFRICAN RICE kusaidia kupata  aina mpya ya mbegu ya mpunga inayoweza kustahimili madhila ya mabadiliko ya tabia nchi lakini pia utawajengea uwezo watafiti na  kuwezesha upatikaji wa vifaa na miundombinu ya utafiti.

Hayo yameelezwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalamu Profesa Maulid Mwatawala wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa kujadili mafanikio yaliyopatikana katikia kutekeleza mradi huo wa CLIMATE-SMART AFRICAN RICE katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

SUA

Aidha Profesa Maulid Mwatawala amesema kuwa Chuo kimekuwa kikishirikiana na  taasisi mbalimbali katika  kufanya utafiti wa zao la mpunga na sasa zipo baadhi ya mbegu ambazo tayali zimeshaanza kutumiwa na wakulima  na zimeonyesha tija katika kuzalisha mazao mengi mashambani.

“Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kina mchango mkubwa na wa muda mrefu kwa sababu kwanza tumeshirikiana na taasisi nyingine kufanya tafiti ya aina mbalimbali za mpunga ambazo zipo sokoni lakini pia kuna aina za mpunga ambazo zimetokana moja kwa moja na watafiti toka SUA. Tuna aina mbili za mbegu ambazo zimesajiliwa moja ni mwangaza na nyingine ni kalalu ni mbegu ambazo zipo na zina sifa ya ukinzani dhidi ya wadudu pamoja na magonjwa ya mpunga”. amesema Prof. Maulid Mwatawala.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa CLIMATE-SMART AFRICAN RICE Profesa Susan Nchimbi Msolla amesema maeneo mengi yanayolimwa mpunga nchini yanachangamoto ya kujaa maji na kusababisha wakulima wengi wa zao hilo kushindwa kuvuna mazao  yao hususani wakulima wanaopanda mpunga kwa kusia hivyo mradi huo sasa unaenda kujibu changamoto hizo ambazo zinasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunachokifanya sasa ni kujaribu kutafuta aina mpya ya mpunga ambayo itakuja kujibu changamoto za mafuriko  na mabadiliko ya tabia nchi  na tayari huko wenzetu kwenye nchi za Asia na Ufilipino wamejaribu na wameona nyingine  hata maji yakiwa mengi  na hata yakitoka au yakipungua zile mbegu zinaendelea kustaimili kwa hiyo na sisi huku tunataka tujaribu  na tayari tumefikia pazuri,  tunaamini tutafanikiwa” amesema Profesa Nchimbi

Pia  ameongeza kuwa Mradi huo utaambatana na mafuzo ya muda mfupi yatakayotolewa kwa Wanafunzi watatu toka shahada ya uzamili, wawili toka shahada ya umahiri pamoja na wana Sayansi mia moja (100) kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na mradi huo kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimbali za kisasa za uzalishaji wa mpunga na jinsi ya kuhifadhi mazao baada ya kutoka shambani.

Mradi wa CLIMATE-SMART AFRICAN RICE unatekelezwa na  Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Copenhagen cha nchini Denmark, Taasisi ya Utafiti wa Mpunga IRRI pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Kwa lengo la kupata mbegu bora za mpunga ambazo zinaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hususani mafuriko yanayopelekea kuongezeka magadi chumvi kwenye mashamba ya mpunga.

Habari: Winfrida Nicolaus -SUAMEDIA

Picha: Vedasto George - SUAMEDIA

Share this page