Umoja wa Wakulima Msoga watembelea SUA kujifunza kilimo cha kisasa

Siku ya Jumamosi, Tarehe 10 Septemba 2022, Umoja wa Wakulima wa Umwagiliaji Msoga (UWAWAUM) kutoka Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani walitembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa lengo la kujifunza na kujionea kwa macho shughuli mbalimbali za kilimo hususan kilimo cha mboga.

SUA

Wakulima hao wakiwa wameambatana na viongozi wao walipokelewa na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda ambaye pamoja na mambo mengine aliwasihi waendelee kushirikiana na SUA katika shughuli zao za kilimo pindi watakapo wahitaji lengo likiwa ni kuinua Kilimo nchini na kukifanya kuwa endelevu.

Profesa Chibunda amesema ni vyema kukifanya kilimo kuwa cha kisasa kwa kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo hasa katika matumizi ya Miundombinu ya umwagiliaji na kuondokana na dhana ya kutegemea mvua pekee kwaajili ya kilimo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWAWAUM Bw. Joel Yohana Kipandwa amesema ziara yao ndani ya SUA ni yamafanikio makubwa  kwani imewawezesha kujionea na kujifunza mambo mbalimbali katika kilimo hivyo kupitia ziara hiyo wataenda kuwa chachu na kuhakikisha wanatumia mafunzo waliyopata kuboresha Miradi yao ya kilimo waliyonayo .

Bw. Gerald Francis Muyuwa, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa UWAWAUM yeye amesema uwepo wa Taasisi kama SUA nchini ni fursa kubwa kwa wakulima kama wao, hivyo kupitia kile walichokiona na kujifunza chuoni hapa wameahidi kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wakulima kutembelea SUA ili kujifunza hivyo kupitia mafunzo watakayoyapata yatawasaidia kukifanya kilimo chao cha Asili walichokizoea kuwa cha kisasa na chenye Tija.

Naye Bi. Rehema Hamisi Mtendaji wa Kijiji cha Msoga amesema kuwa Elimu haina mwisho hata mkulima anatakiwa ajifunze kila siku lengo likiwa ni kujikwamua kiuchumi na matamanio yao ni kuona wakulima wa Msoga wanalima kilimo chenye Tija na cha Kisasa kwaajili ya maendeleo hivyo SUA imekuwa sehemu sahihi ya wao kuja kujifunza na wamejionea kwa macho mambo mazuri na ya faida kwao kama wakulima.
 


Habari na Picha: Winfrida Nicolaus - SUAMEDIA

Share this page