Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea na jitihada zake za kuunga mkono sera za nchi na mwelekeo wa taifa kuelekea kukuza uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha kinatoa wataalam wenye ujuzi na maarifa ambayo yatasaidia katika kuinua uchumi wa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vimeanzishwa nchini.
Hayo yamebainishwa na Prof. Japhet Kashaigili ambaye ni Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA wakati akifungua mafunzo ya kongano la nguo mjini Morogoro yaliyo ratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia kitengo cha Sayansi ya Mlaji yaliyo wajumuisha mafundi nguo na wabunifu wa mavazi kwa mkoa wa Morogoro.
"Kituo cha Ubunifu Kilichoko katika Kurugenzi hii kimejikita katika kutoa elimu ya bunifu mbalimbali, hati miliki, tafiti, uhaulishaji wa Teknolojia kwa wanafunzi, watafiti na wajasiriamali wa viwanda vidogo na vya kati na Dhumuni kubwa la kituo hiki ni kutoa maarifa shirikisha , kuchochea ubunifu kwa kuunganisha watu wenye fikra na mtizamo sawa ndani na nje ya Chuo cha Sokoine cha Kilimo, lakini Kwa ujumla kituo hiki kinalenga kujenga bunifu na ujasiriamali kwa kuboresha mahusiano kati ya chuo, viwanda na taasisi nyingine za nje" Alifafanua Prof.Kashaigili
Prof.Kashaigili ameongeza sambamba na kitengo cha bunifu kilichoko katika kurugenzi, kitengo cha Sayansi ya Familia na Walaji kilichoko Ndaki ya Kilimo, kinalenga kuboresha bunifu, ujuzi, maarifa, tafiti zinazosaidia watu kufanya maamuzi yanayolenga ustawi, mahusiano, na rasilimali ili kuweza kufikia maisha bora zaidi.
Aidha Kashaigili amesema kitengo cha Sayansi ya Familia na Walaji kinajikita katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na ubunifu na ushonaji mavazi, mpangilio na upambaji wa ndani ya nyumba pamoja na masuala yanayohusisha sayansi ya walaji.
"Mafanikio ya viwanda hivi ikiwemo viwanda vya Kongano la nguo Morogoro (KONGUMO) yanategemea namna viwanda hivi vinavyoweza kuboresha teknolojia na kujenga uwezo na hatimaye kuzalisha aina nyingi zaidi za bidhaa za kuuza ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza tija na faida kwa kutumia kiasi kidogo cha mtaji" Alifafanua Prof.Kashaigili
Mary Marcel, Mhadhiri na Mbobezi wa masuala ya ubunifu wa mavazi,Utengenezaji wa samani na mapambo ya ndani kutoka SUA
Kwa upande wake, Mary Marcel ambaye ni Mhadhiri na Mbobezi wa masuala ya ubunifu wa mavazi,Utengenezaji wa samani na mapambo ya ndani kutoka SUA amesema kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na mafundi nguo hapa nchini katika utengenezaji wa mavazi Chuo kupita washirika wake kimeona kuna haja ya kuwaongezaea ujuzi katika kazi yao ya ubunifu wa mavazi ili iweze kuwa na thamani zaidi.
"Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo zamani kilikuwa kinajulikana kinahusika na kilimo tu lakini hivi karibuni kuanzia mwaka 2010 Chuo kiliweza kujipambanua na kwenda kwenye Nyanja nyingine ambazo zinamuhusu zaidi mlaji, sasa kupitia kitendo cha cha sayansi ya mlaji wakajiweka zaidi kwenye ubunifu wa mavazi tukitambua mavazi ni kitu muhimu kwa binadamu na tukasema isiwe tu bora mavazi lakini lazima vazi liwe la ubunifu ili mtu anavyo vaa vazi na muonekano wake uwendane, kwaiyo kupitia kitengo hichi cha ubunifu tukatambua kuwa kuna mafundi ambao wanasaidia kushona haya mavazi ndomaana leo tunawapa mafunzo" Alisema Mary Marcel
Naye Robert Joseph, Mwenyekiti wa KONGUMO la nguo Manispaa ya Morogoro akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine amesema matarajio yao baada ya mafunzo ni kukakikisha wanafanya ubunifu wa mavazi wenye tija na wenye kulenga soko la ndani nanje ya nchi huku akiongeza kuwa mafunzo hayo yatawabadilisha mafundi katika kutekeleza kazi zao na kuongeza uaminifu kwa wateja
Robert Joseph Mwenyekiti wa KONGUMO la nguo Manispaa ya Morogoro