SUA Yaishukuru Serikali

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na Jaji mstaafu, Mhe. Mohamed Othman Chande, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Ruzuku na Fedha za maendeleo inayotoa kwa Chuo. 

SUA

Jaji mstaafu, Mhe. Mohamed Othman Chande

Mhe. Chande ametoa kauli hiyo Mei 27, 2022 wakati wa Mahafali ya 39 ya Katikati ya mwaka ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Nelson Mandela Freedom Square Kampasi ya Solomon Mahlangu Mazimbu, Morogoro.

Amesema kwa kipindi cha miezi 6 tangu kufanyika mahafali ya 38 mwezi Novemba 2021, Baraza lake limeweza kutekeleza majukumu mbalimbali yakiwemo kusimamia Mpango Mkakati wa 4 wa mwaka 2021 ambao umetekelezwa kwa sh. bilioni 54.2 pamoja na kupitisha marekebisho ya viwango vya ada na gharama nyingine kwa Program za Shahada za Uzamili. 

“Chuo kimeendelea kunufaika sana kutokana na mikataba iliyosainiwa na Taasisi pamoja na wadau wa maendeleo bila kusahau mchango mkubwa unaotolewa na Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan” alisema Mhe. Chande

Aidha aliongeza kuwa kutokana na mchango na makubaliano hayo Chuo kimejenga uwezo wa Rasilimali watu, Miundombinu, Vitendea kazi, Utafiti, Mafunzo, Ugani na manunuzi ya vifaa na zana za kufundishia kwenye madarasa, maabara na karakana za uhandisi. 

Prof. Raphael Chibunda

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda, amesema Chuo kimeendelea kuaminika nchini kwa kuweza kutoa nafasi mbalimbali za watumishi wa Serikali na Sekta binafsi ambapo watumishi 10 kutoka SUA waliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye Taasisi, Wizara, na Mashirika mbalimbali, ambapo baadhi ya teuzi hizo zilifanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mbali na mafanikio hayo, pia Serikali yetu tukufu chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan imekipatia Chuo chetu nafasi za ajira 140 zikiwemo nafasi za Wanataaluma 94 na nyingine za Wafanyakazi wa kawaida, hivyo mchakato wa kuzingatia nafasi hizo unaendelea” alisema Prof. Chibunda

Akizungumzia Changamoto Prof. Chibunda amesema Chuo kina upungufu wa miundo mbinu ya kufundishia, mabweni ya kulala wanafunzi na nyumba za watumishi. 

Jumla ya wahitimu 209 wakiwemo wanaume 147 na wanawake 62 walitunukiwa Shahada mbalimbali na Mgeni rasmi katika Mahafali hayo ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba.Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba

 

Share this page