SUA na NEMC Yapanda Miti Zaidi ya 45,000 katika Vyanzo vya Maji Nyanda za Juu Kusini

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mzingira (NEMC) wamepanda miti rafiki na maji zaidi ya 45,000 kwenye vyanzo vya maji vya Mto Mbarali unaochangia maji yake kwenye Mto Ruaha Mkuu, Bwawa la Kidatu na Bwawa la Mwalimu Nyerere kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutunza vyanzo vya maji nchini.

SUA na NEMC Yapanda Miti Zaidi ya 45,000 katika Vyanzo vya Maji Nyanda za Juu Kusini

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Wanging’ombe Bi.Veronica akizindua rasmi zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji cha Mto Mbarali katika kijiji cha Mdandu.

Akizindua zoezi hilo kupitia Mradi wa Tathimini ya maji kwa mazingira (EFLOWS) katika Kata ya Mdandu Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi. Veronica Sanga aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya Mhe. Claudia Kitta amesema zoezi hilo linazidi kuchochea jitihada za Wilaya hiyo na Mkoa katika kuhifadhi vyanzo vya maji na mito ili kuhakikisha mtiririko endelevu wa maji kuelekea bwala la kufua umeme la Kidatu na Mwl. Nyerere ambayo yanategemea maji kutoka nyanda za juu kusini.

“Sisi kama Serikali tumekuwa tukichukua hatua kali kwa watu wote waliobainika kufanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji na ndani ya miti 60 kandokando ya mito, na kwa jitihada hizi zilizofanywa na SUA kwa kushirikiana na NEMC, tunakuja kwa kasi kubwa zaidi maana tusipotunza vyanzo hivi vya maji maana yake maji kwenye bwala la kufua umeme la Kidatu, Mtera na jipya la Mwl. Nyerere hayatapata maji na hivyo nchi itakosa nishati muhimu ya umeme na hivyo kuharibu shughuli mbalimbali za kiuchumi” alisisitiza Bi Veronica.

Aidha ameeleza kuwa zimewekwa sheria katika vijiji vyote kuhakikisha utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji unakuwa ni ajenda ya kudumu kwenye vikao vyote na amewataka Wananchi wanaoishi kandokando ya vyanzo hivyo kufuata sheria na kuunga mkono jitihada za Serikali na wadau wengine kuhifadhi mazingira ili kuifanya Tanzania kuwa ya kijani kwa kuepusha nchi kuwa jangwa.

Kwa upande wake Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitalamu, Prof. Maulid Mwatawala amesema kutokana na utafiti uliofanywa na Watafiti kutoka SUA na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamefanya utafiti kubaini aina bora za miti ambayo ni rafiki wa mazingira na vyanzo vya maji na kisha kuiotesha kwa ajili ya kurejesha uoto kwenye vyanzo kama sehemu ya mfano katika Wilaya ya Wanging’ombe na Mbarali.

3 (9)

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cah Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Walad Mwatawala akitoa salamu za SUA kwenye uzinduzi wa zoezi hilo.

“Tunatambua kuna miti mingi lakini mingine ni rafiki wa mazingira, Vyanzo vya maji, lakini pia ipo ambayo inakausha maji, tunafurahi kukujulisha mgeni rasmi kuwa Mradi huu umefanya utafiti na utambuzi na umeotesha miti mizuri rafiki wa maji na tunafurahi sisi kama SUA tunashiriki na kutoa mchango katika uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kwenye eneo hili la nyanda za juu kusini ambalo ndio kitovu cha maji kwenye mito mikubwa na muhimu kwa ustawi wa taifa letu” alieleza Prof. Mwatawala.

Aidha Prof. Mwatawala amewashukuru watafiti wenza kwenye mradi huo kutoka NEMC kwa ushirikiano mkubwa ambao wanautoa katika utekelezaji wa mradi huo muhimu wenye faida kubwa kwa Taifa na katika kufanya tathimini hiyo ya mtiririko wa maji kwa mazingira kuelekea bahari ya Hindi na katika miradi mikubwa ya kimkakati ya Taifa.

Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa EFLOWS kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Cha kilimo (SUA) Prof. Japhet Kashaigili amesema kupitia utafiti walioufanya wakati wa kiangazi na masika wamebaini uharibifu mkubwa wa vyanzo hivyo na kando ya mito, hivyo upandaji huo wa miti rafiki kwa mazingira ni sehemu ya mchango wa Utafiti katika kurejesha vyanzo hivyo katika uasili wake.

“Kwa kuanzia sisi kama mradi tumefanikiwa kuotesha miche rafiki kwa maji zaidi ya 45,000 ambayo uzinduzi wake ndio tunaufanya hapa leo katika Wilaya ya Wanging’ombe na zoezi litaendelea hadi katika Wilaya ya Mbarali ambapo mradi huu unatekelezwa na katika kupata aina bora za miti tumeshirikiana na TFS, Wataalamu wa Bodi ya Bonde la Mto Rufiji pamoja na Wananchi wenyewe ambao ndio wazawa wa maeneo haya, sisi tunaunga mkono juhudu za Rais na Makamu wa Raisi wetu Mhe. Philip Mpango aliyezindua zoezi la upandaji miti kwenye vyanzo vya maji nyanda za juu kusini, alifafanua Prof. Kashaigili.

4 (7)

Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS kutoka SUA Prof. Japhet Joel Kashaigili akieleza malengo ya mradi huo, kazi walizozifanya na uhusiano wake na zoezi hilo la upandaji wa miti rafiki na maji kwenye vyanzo vya mito.

Prof. Kashaigili amesema pamoja na utafiti huo, lakini pia wameendelea kushirikiana na jumuiya zote za watumia maji na kuwajengea uwezo wa namna za kuhifadhi mito na vyanzo vya maji pamoja na kusomesha wataalamu katika ngazi ya Shahada ya Uzamili kutoka NEMC ambao wamejikita pia kufanya tafiti kuangalia uoto wa asili katika mito na vyanzo vyake, Ikolojia, viumbe wanaotegemea maji, Afya ya mto na Mopholojia yake ambao watakuwa na mchango mkubwa kwa taifa.

Nae Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamzi wa Mazingira (NEMC), Bi. Rose Sallema Mtui ambaye ni mtafiti mwenza wa Mradi kutoka (NEMC) amesema hivi sasa kumekuwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi nchini ambayo yanasababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu kwenye mazingira.

 “Kwa mujibu wa sheria sisi (NEMC) kama msimamizi mkuu wa Mazingira katika nchi yetu tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa sheria ya mazingira inazingatiwa katika maeneo ya Utafiti, ufuatiliaji na tathimini za athari kwa mazingira kwa kushirikiana na Sekta, Taasisi na Wizara mbalimbali nchini, lakini kila Mwananchi analo jukumu la kutunza mazingira na rasilimali maji kwaajili ya maisha na maendeleo endelevu” alifafanua Bi. Rose.

5 (6)

Mtafiti wa mradi wa EFLOWS kutoka NEMC Bi. Rose Sallema Mtui akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira.

Amesema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na wadau na Serikali, bado kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo kilimo kisicho endelevu hasa vinyungu, ufugaji usio endelevu,Ukataji miti hovyo,umwagiliaji usiofuata sheria ambavyo kwa pamoja vinaathari katika mfumo wa utiririshaji maji.

Nae Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji bwana Florence Mahay aliyemuwakilishaMkurugenzi za Rasilimali za Maji Wizara ya Maji Dkt. George Lugomela amepongeza kazi nzuri inayofanywa na watafiti wa SUA na NEMC na kusema kuwa uendelevu wa rasilimali za maji unategemea sana utunzaji wa vyanzo,mito na upandaji wa miti kwenye maeneo hayo.

“Kazi ya Bodi ya maji ya Bonde la maji la mto Rufiji ni usimamizi wa rasilimali za maji na kazi yetu ya kwanza ni kujibu swali kwamba katika huu mfumo wa wa mto Rufiji kuna rasiliamali ya maji kiasi gani na jukumu hili ndilo linatufanya tuwe na unahusiana moja kwa moja na Mradi na kazi wanazozifanya maana zinasaidia kujibu swali hilo kikamilifu kupitia utafiti” alieleza Bwana Mahay.

6 (4)

Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Bwana. Florence Mahay akiwasilisha salamu za Mkurugenzi za Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt. George Lugomela wakati wa uzidnuzi huo.

Amesema mto Rufiji unazalisha kiasi cha lita za ujazo bilioni 31 kwa mwaka katika mwaka ambao mvua zinakuwa za kawaida na takwimu hizo zinapatikana kupitia taarifa za hali ya hewa na mtiririko wa maji kwenye mito na baada ya kupata majibu wanafanya kazi nyingine ya kugawa maji hayo kwakuwa rasiliamali maji ni kichocheo cha maendeleo ya sekta zote na bila maji hakuna sekta inayoweza kuendelea.

Mradi huu unatekelezwa na Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira na unatekelezwa katika dakio la mto Mbarali katika bonde la mto Rufiji kwa ushirikino na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, Jumuiya za watumia maji, TFS, Wilaya ya Mbarali na Wanging’ombe na jamii, kwa ufadhili wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) na kutelezwa kupitia Sekretarieiti ya Azimio la Nairobi.

7 (4)

Madiwani wa kata ya Igima Paulina Samatta, Anthony Mawata wa kata ya  Igwachanya, Wiston Mbilinyi  wa kata ya Kidugala na mwenyeji wao Annapendo Gombela wa kata ya Mdandu wakishiriki katika zoezi la upandaji miti kwa niaba ya madiwani wengine wa halmashauri hiyo.

8 (2)

Wasimamizi wa mradi huo wa EFLOWS kushoto ni mtafiti kutoka NEMC Bi. Rose Sallema Mtui katikaki ni mtafiti mkuu wa mradi kutoka SUA Prof. Japhet Kashaigili na kulia ni Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Rufiji Bwana. Florence Mahay wakishiriki katika zoezi la upandaji miti.

9 (1)

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Wanging’ombe Bi.Veronica Sanga akikabidhi moja ya Mzinga Nyuki na Vifaa vingine kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji ya Mbumtilu bwana Asheri Kilasi kwa niaba ya Jumuiya zingine.

15

16

Wananchi na wadau wengine wakishiriki kwenye zoezi la uzinduzi na upandaji wa miti rafiki na maji kwenye vyanzo vya maji.

Share this page