Serikali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwa chanzo cha uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki na hivyo kuwapunguzia wafugaji changamoto ya upatikanaji wa vifaranga hivyo.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 7, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo wakati alipotembelea Banda la SUA katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mjini Morogoro.
Baada ya kupata maelezo ya namna vifaranga vya samaki aina ya sato vinavyozalishwa kwa kutumia Maabara inayotembea maalum kwa utotoreshaji wa vifaranga vya samaki Mhe. Jafo amesema hatua hiyo ya utotoreshaji wa vifaranga inayofanywa na SUA itaondoa malalamiko ya wafugaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa na kilio cha sehemu sahihi ya kupata vifaranga vilivyo bora.
“Profesa naomba nikupongeze sana hasa kwa upande wa samaki, watu wengi sasa hivi wanatamani kuacha kuvua kupitia katika vyanzo vya bahari moja kwa moja ama mito moja kwa moja wanatamani watengeneze bwawa nyumbani kwa ajili ya samaki lakini changamoto kubwa ambayo inajitokeza sasa hivi ni ukosefu wa vifaranga”, amesema Waziri Jafo.
Amefafanua kuwa “kuna vitu viwili ukosefu wa vifaranga au ukosefu wa taarifa sahihi za vifaranga wanapatikana wapi, kwa hiyo Profesa nikupongeze tena kwa sababu hata mimi ni mmojawapo wa watu wanaofuga samaki na samaki wangu huwa nakuja kuwachukua hapa hapa Morogoro sasa nikiona Chuo changu cha SUA kinazalisha vifaranga napata faraja sana ”.
Maonesho ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nanenane yalianza rasmi Agosti 1, 2023 na yatafungwa Agosti 8, 2023 ambapo Kitaifa yanafanyika mkoani Mbeya.