Nane nane 2022: Wafugaji washauriwa kuwekeza kwenye ufugaji wa samaki

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia Ndaki ya Kilimo, Idara ya Sayansi ya Wanyama, Viumbe Maji na Malisho imeshauri jamii hususani wakulima na wafugaji kuwekeza kwenye ufugaji wa Samaki kwa kuwa ufugaji wa samaki kwa sasa una soko kubwa na umekuwa ni chanzo cha ajira kwa watu wengi.

SUA

Akiongea na ofisi ya Mawasiliano na Masoko katika banda la idara hiyo kwenye viwanja vya maonesho ya Nane nane (viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere) siku ya Jumanne tarehe 2 Agosti, 2022 Bw. Rashid Lipoyola ambae ni mwanafunzi wa mwaka wa pili shahada ya Sayansi ya Viumbe Maji amesema Soko la Samaki linazidi kukua siku hadi siku, wafugaji wamekuwa hawapati matatizo pindi inapofikia wakati wa mauzo lakini cha msingi na cha kuzingatia ni wao kuhakikisha wanafuga kwa kufuata ushauri wa kitaalamu ambao SUA wanautoa.

Aidha Bw. Lipoyola ametoa wito kwa jamii kufuga Samaki wa Mapambo ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa ni kivutio na wanachangia kuleta faraja hata pale unapokuwa na msongo wa mawazo

“Samaki wa Mapambo unapokuwa nao nyumbani wanasaidia kuleta utulivu wa akili kutokana na rangi zao, faida nyingine ni kwa watoto kwani samaki wa mapambo ukiwa nao nyumbani wanasaidia kuwafanya watoto kuzoea mapema Viumbe waishio kwenye maji”, amesisitiza Bw, Lipoyola.

SUA inazalisha vifaranga vya samaki na kutoa elimu bora jinsi ya kutunza samaki hao, lakini pia inazalisha chakula cha samaki majani aina ya Azola ambayo ni mojawapo ya chakula kizuri cha Samaki na Mifugo mingine kama vile Kuku, Ng’ombe na Wanyama wengine wafugwao kwa kuwa Azola ina Protini nyingi inayowafanya wanyama kukua kwa haraka.





Share this page