Nane Nane 2022: Rai yatolewa kwa Serikali tafiti za SUA zipewe kipaumbele

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda ametoa rai kwa Serikali kuhakikisha wanazipa kipaumbele Tafiti zinazofanywa na Vyuo vikuu Tanzania ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kila Mwaka ili kuisaidia jamii na kuleta Maendeleo kwa Taifa.

SUA

Mhe. Mizengo Pinda amesema hayo akiungumza na wananchi siku ya Alhamisi, tarehe 4 Julai, 2022 wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 29 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro.

Pia amesema kuwa Serikali inapaswa kuwapa kazi Vyuo Vikuu nchini ikiwezekana kila mwaka vikusanye Tafiti angalau tatu au tano ambazo wataziona zina tija kubwa katika kuleta mabadiliko kwa watanzania.Tafiti hizo pia zinatakiwa zionekane zinaenda mahali gani na zimesaidia jamii kwa kiasi gani, kwakua tafiti zinazofanywa na Vyuo kama SUA na vingine zina mambo makubwa na mazuri ambayo Serikali ikiyatumia na kuyapeleka kwa jamii itasaidia kuleta tija kwa Taifa.  

“Tuna Vyuo kama SUA hawa watu ukienda na kusikiliza Tafiti zao wana mambo makubwa na mazuri na watakwambia katika tafiti liko hili na kwenye tafiti hii kuna hili lakini nadhani hata wao watakuwa wanajiuliza sasa hizi tafiti zinasaidia wapi na kwa kiasi gani, hivyo nilikuwa nawaza kwanini hivi Vyuo tusiwape kazi. mfano SUA kila mwaka watuletee tafiti tatu au tano ambazo ninyi mnaona zina tija katika kuleta mabadiliko kwa Watanzania”, amesema Mhe. Mizengo Pinda

Aidha amevitaka Vyuo Vikuu vyote kupitia Tafiti zao kwenda Serikalini na kuelezea vitu ambavyo wamevifanyia Tafiti na kwa namna gani zitasaidia jamii na kwenye mipango ya Serikali. 

Sekta ya Kilimo ni Mhimili Muhimu katika kuleta Maendeleo kwa Taifa hivyo ni vizuri kupima jamii imesaidika vipi kupitia Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi lengo likiwa ni kuhamasisha jamii na kuleta maendeleo kwa Taifa kupitia Kilimo, Ufugaji, Uvuvi pamoja na Misitu. 


 

Share this page