Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kupokea Watafiti, Wanasayansi na Watalii kutoka nchi mbalimbali duniani wanaokwenda kujifunza, kufanya tafiti na utalii juu ya masuala mbalimbali ya Misitu na Viumbe wengine wengi kwenye Msitu wa Hifadhi Mazumbai ambao haujawahi kuguswa toka miaka ya 1,800 enzi za ukoloni wa Mjerumani.
Msitu huu unapatikana Jimbo la Bumbuli Mkoani Tanga.
Hayo yamebainishwa na Mhadhiri Msaidizi na Kaimu Mwangalizi wa Msitu huo na kituo hicho cha Mafunzo cha SUA Mhifadhi Chamalindi Bugingo Muriga wakati akiongea na Waandishi wa habari waliokwenda kutembelea kituo hicho kuona vivutio mbalimbali vya kipekee na viumbe vinavyopatikana kwenye msitu huo.
‘’Kazi kubwa inayofanywa na Menejimenti ya SUA katika kutunza msitu huu wa asili ndio inayowavutia wanasayansi wengi duniani kuona hapa ndio mahali sahihi kwa wao kuja kujifunza na kufanya tafiti za misitu na viumbe hai mbalimbali wa kipekee wanaopatikana kwenye msitu wetu, Msitu huu haujawahi kuguswa kwa shughuli yoyote ya kibinadamu zaidi ya miaka 200 na hivyo kupelekea kuwa na miti mikubwa ambayo pengine haipo maeneo mengine duniani‘’ alieleza Mhifadhi Chamalindi.
Aidha amesema, kutunzwa vizuri kwa msitu huo kunasaidia kuwa sehemu nzuri ya benki ya mbegu za miti mingi ya asili ikiwemo mimea dawa,Miti ya mbao na matunda ambayo huwezi kupata kwenye misitu mingine ya asili nchini na hii kuwa kimbilio la watafiti wengi wa masuala ya misitu, ndege, uyoga, wanyama,vyura na vinyonga.
‘’Kwenye msitu huu kuna miti yenye maumbo mbalimbali ya kuvutia ikiwemo miti aina ya Mibokoboko Entandrophragma deiningelii yenye mizizi mikubwa zaidi ya mita 2 kutoka ardhini ambayo imetengeneza ukuta kama nyumba, mingine mikubwa ambayo kiuno chake kuweza kuukumbatia hadi muungane watu wazima saba, na mingine yenye pango Mtonho/Mtonto Cylicomorpha parviflora ‘’ alifafanua Mhifadhi Chamalindi.
Mhadhiri msaidizi na Kaimu Mwangalizi wa Msitu huo na kituo hicho cha mafuzno cha SUA Mhifadhi Chamalindi Bugingo Muriga wakati akiongea na Waandishi wa habari ndani ya msitu huo.
Kwa upande wake Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Agnes Sirima aliyeambatana na wanahabari hao amesema msitu huu wenye ukubwa wa Hektali 320 ni fahari ya Tanzania kwa kuwa ndio msitu pekee mkubwa na ulioshona ambao unamilikiwa na SUA.
‘’Pamoja na kutumiwa na Wanasayansi na Watafiti wengi duniani lakini tunautumia kwenye kufundisha Wanafunzi wa shahada mbalimbali za Misitu, Uhifadhi, Mazingira na Italii na hivyo kituo hiki kuwa na mchango mkubwa kwa Chuo kwenye kutoa Mafunzo kwa Vitendo kwa wanafunzi wetu‘’alieleza Dkt. Sirima.
Aidha Dkt. Sirima akieleza historia ya msitu huo amesema inaanzia miaka ya 1800, ambapo Wajerumani walianzisha kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo Mkonge kwenye maeneo ya Usambara ambapo pamoja na kilimo kilichogharimu kufyeka baadhi ya maeneo ya misitu, waliweza kuhifadhi misitu ikiwemo Msitu wa Hifadhi Mazumbai.
Amesema mnamo mwaka 1896, Wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya Kahawa chini ya kampuni iliyojulikana kama West Plantambayo msimamizi mkuu alikuwa Karl Peters lakini mwaka 1994 waliachana na kilimo cha Kahawa na kuanzisha kilimo cha mazao mengine ikiwemo Chai, Kwinini, Miwati na matunda kama apple, peaches, pears na plums.
‘’Wajerumani waliposhindwa vita na Waingereza mwaka 1918, kampuni ya West Plant ilichukuliwa na wawekezaji Waswisi na Waingereza ambapo mwaka 1921 Kampuni ya West Plant ilibadilishwa jina na kuitwa Amboni estates chini ya Msimamizi mkuu, Mswisi alijulikana kwa jina la Hugo Tanner na baada ya kustaafu, mwaka 1933, Amboni estates walimuuzia Hugo Tanner Mashamba na Misitu ya Mazumbai yenye ukubwa wa hektari 960 na mwaka 1940 Tanner alijenga eneo la Makazi Mazumbai na majengo yake yapo hadi leo‘’ alieleza Dkt. Sirima.
Rasi huyo wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii amesema Hugo Tanner pamoja na wafanyakzi wake 103 waliunda umoja uliojulikana kama Sagara group mwaka 1964 na mnamo mwaka 1968, John Tanner mtoto wa Hugo Tanner aliugawa msitu wa Mazumbai kwa Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM na akaomba msitu hui uhufadhiwe kwa ajili ya mafunzo na utafiti.
Dkt. Sirima amesema historia inaonesha katika eneo la hektari 640 ambazo zilikuwa na mashamba na mistu ziligawiwa kwa waliokuwa wafanyakazi wake kama kiinua mgongo na Baada ya Tanganyika kuwa nchi huru, John Tanner alinyimwa kibali cha kuendelea kukaa nchini na ndipo aliamua kugawa eneo la makazi kwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam itumike kama mahali pamalazi kwa wageni mbalimbali watakaotembelea msitu.
Watalii wakipata picha kwenye moja ya miti yenye mizizi mikubwa kama ukuta.
Menejimenti ya Msitu wa mazumbai (UDSM) ulikuwa chini ya kilichokuwa Kitivo cha Kilimo, Misitu na Tiba ya Wanyama kilickokuwa Morogoro hadi mwaka 1984, kitivo hiki kilipopandishwa hadhi na kuwa Chuo Kikuu kamili kwa jina la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na ndipo iliamuliwa kwamba SUA itakuwa msimamizi mkuu wa Msitu wa Hifadhi Mazumbai na pia watafiti toka (UDSM) wataruhusiwa kufanya utafiti msituni bila kulipa gharama za kuingia msituni.
Muonekano wa eneo la ofisi za Kituo na msitu wa Hifadhi wa Mazumbai.