Mradi wa Cystnet Afrika Wawasilisha Matokeo ya Utafiti wa Minyoo Tegu ya Nguruwe Tanzania

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Taasisi ya Utafiti wa magonjwa ya Binadamu NIMR, wamefanya utafiti na kuja na mapendekezo yatakayowezesha kumaliza tatizo la minyoo tegu ya Nguruwe ambayo ina madhara makubwa kwa afya ya Binadamu na Wanyama.

Mradi wa Cystnet Afrika Wawasilisha Matokeo ya Utafiti wa Minyoo Tegu ya Nguruwe Tanzania

Picha ya Pamoja ya wadau walioshiriki warsha ya kupokea na kujadili mrejesho wa matokeo ya utafiti kuhusu namna ya kudhibiti mnyoo tegu wa nguruwe Tanzania kupitia mradi wa CYSTINET Afrika.

Akifungua warsha hiyo ya kujadili mrejesho wa matokeo ya utafiti kuhusu namna ya kudhibiti minyoo tegu wa Nguruwe Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Ezron Nonga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia sekta ya mifugo Bwana Tixon Nzunda amesema Serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha matokeo ya utafiti huo yanatumika na kuleta tija kwa taifa.

“Tunapokuwa tunahitaji kutunga Sera nzuri na kutekeleza mipango mbalimbali ya Wizara yetu tunathamini sana matokeo ya tafiti maana yanatusaidia kupata uthibitisho na ushahidi ambazo zinawezesha utengenezaji na utekelezaji wa miapango yetu kama wizara kwa maaslahi mapana ya sekta ya mifigo maana yake huwezi kutengeneza Sera nzuri kama huna matokeo sahihi ya utafiti” alisema Prof. Nonga.

2 (5)

Mkurugenzi wa Huduma za mifugo kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Ezron Nonga akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi  anayesimamia sekta ya mifugo Bwana Tixon Nzunda.

Aidha amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022 Tanzania ina Nguruwe milioni 3.4 na inazalisha nyama tani elfu 45 kwa mwaka, nyama ambayo inaonekana kuwa ndio nyama pendwa zaidi kuliko nyama zingine kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni.

Mkurugenzi huyo wa Huduma za Mifugo nchini amesema minyoo tegu ya Nguruwe inachangia ugonjwa wa kifafa kwa binadamu kwa zaidi ya asilimia 30 na hii ni kwa maeneo ambayo yanafuga Nguruwe kiasili nje ya mabanda kwa kuwaachia kujitafutia chakula wenyewe mitaani.

Akizungumzia matokeo hayo ya ujumla wa tafiti hizo zilizofanyika kwa zaidi miaka 26 Mkurugenzi wa Mtandao wa kisayansi wa CYSTINET Afrika Kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Helena Ngowi amesema baada ya kazi kubwa ya utafiti kwenye maeneo mbalimbali nchini na kupata matokeo wameona ni vyema sasa matokeo hayo na mapendekezo yao wayawasilishe mbele ya wadau wote muhimu ikiwemo Wizara ili waone namna ya kuyatumia katika kutunga sera zitakazosaidia kutokomeza Minyoo tegu hiyo.

“Baada ya kazi hii sasa tumekuja na mapendekezo kadhaa ambayo tunaamini yakitekelezwa kwenye kipindi cha miaka mitano tunaweza kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la Minyoo tegu ya Nguruwe na kusaidia Jamii kufanya ufugaji bora na kula nyama salama ambayo haiwezi kuleta athari kwa binadamu” alieleza Prof. Ngowi.

Ameyataja miongoni mwa mapendekezo hayo ni kutengeneza Sera na miongozo au sharia ambayo itawafanya wafugaji wote wa Nguruwe kufugia ndani ya mabanda badala a kuwaacha mtaani wajitafutie chakula hali ambayo inasababisha mzunguko wa Minyoo tegu kuendelea.

Pia Mkurugenzi huyo wa Mtandao wa kisayansi wa CYSTINET Africa amefafanua pendekezo linguine la utafiti huo kuwa ni kuwepo kwa machinjio ya Nguruwe kwenye kila miji na vijiji ambavyo vinatumia,Vinafuga au kufanya biashara ya nyama ya Nguruwe ili Nyama hiyo iwe inakaguliwa na wataalamu waliopewa mamlaka ya kukagua usalama wa Nyama kuona kama ni salama na haina minyoo hiyo ili kuzuia jamii kula nyma iliyoathirika.

Aidha Prof. Ngowi amesema kutoka na kuwa na maeneo mengi ambayo watu wanakwenda kula nyama ya Nguruwe wanapendekeza ziwe zinakaguliwa na kuwa safi ili kuondoa namna zozote za uambukizaji wa wa mniyoo hiyo na kuhakikisha inapikwa vizuri katika viwango vinavyotakiwa ili kuweka walaji kwenye mazingira salama wanapokula.

3 (5)

Mkurugenzi wa Mtandao wa kisayansi wa CYSTINET Afrika Kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Prof. Helena Ngowi akiwasilisha wasilisho kuhusu minyoo tegu ya nguruwe na madhara yake Tanzania.

Amesema kwakuwa mayai ya Minyoo ya Tegu wa Nguruwe yameonekana kwenye ardhi kwenye maeneo ya wafugaji wa Nguruwe na yanaweza kuishi kwa muda mrefu kwenye ardhi na yakipata mazingira ya kuanguliwa yanaanguliwa wamependekeza kuwe na maeneo ya maji safi kwaajili ya kunawa mikono mashuleni na kwenye masoko ili kuepuka kula mayai hayo ya tegu kutokana na vumbi au matunda nambogamboga sokoni.

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na insia Prof. Samweli Kabote aliyemuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema kwa upande wa SUA mradi huo umejikita katika kufanya uchunguzi wa kina wa hali ya maambukizi pamoja na kufungamanisha na utoaji wa elimu ya fya kwa gharama nafuu na kujenga uwezo wa kitaasisi na kimfumo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kupitia mkakati wa afya moja.

4 (4)

Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na insia Prof. Samweli Kabote aliyemuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Kilimo Prof. Raphael Chibunda akitoa salamu za SUA kwenye Warsha hiyo.

“Nchini Tanzania, utafiti huu umeoensha viwango tofauti vya maambukizi ya minyoo tegu kwa Binadamu na kwa Nguruwe lakini pia tumeona jinsi ambavyo binadamu yupo katika hatari ya kubwa ya maambukizi ikiwa hatozingatia usafi na matumizi sahihi ya vyoo au kula nyama ya nguruwe yenye maambukizi” alieleza Prof. Kabote.

Aliongeza “Madhara ya minyoo tegu ni makubwa ikiwemo Kifafa,Kupooza na  upofu hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari na kufanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye utafiti huu ili kuepukana na magonjwa hayo”.

Prof. Kabote amesema kunamahusiano makubwa ya magonjwa hayo yanayotokana na minyoo tegu ya Nguruwe na Maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya binadamu kwakuwa wanatashindwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo na uchumi na kuanzia ngazi yake binafsi hadi Taifa.

Utafiti huo umefanyika kwenye wilaya za mikoa mbalimbali inayosifika kwa ufugaji wa nguruwe ikiwemo Mbulu, Babati, Songwe, Kongwa, Mpwapwa, Mpanda unatekelezwa kupitia mradi wa CYSTINET Afrika kwa ufadhili wa Wizara ya elimu na utafiti ya shirikisho la Ujerumani (BMBF).

 

Na: Calvin Gwabara – Dodoma.

Share this page