Mkuu wa Wilaya ya Morogoro apongeza tafiti mbalimbali zinazofanywa na SUA 

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Wakili Alberto Msando amepongeza tafiti zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwani zinaisaidia serikali kutengeneza sera bora na kurekebisha zilizopo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.

Albert Msando

Mheshimiwa Wakili Alberto Msando akifungua Maonesho na siku ya Ubunifu SUA

Pongezi hizo amezitoa siku ya Jumamosi tarehe 7/05/2022 wakati akizungumza na wanataaluma, wanafunzi, wabunifu na wadau mbalimbali wa Chuo kwenye uzinduzi wa  siku ya Ubunifu iliyofanyika ukumbi wa Nelson Mandela Freedom Square kampasi ya Solomoni Mahlangu Mjini Morogoro. 

Ameipongeza SUA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuzalisha wahitimu ambao wana mchango mkubwa kwa taifa na kwamba wote aliokutana nao wana mawazo ya kujiajiri na kufungua biashara kwenye Kilimo na kufikiria kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.

Aliendelea kusema kuwa watu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wanafikiria na ndio maana anapenda kujifungamanisha nao kwasababu ukikaa na watu wenye kufikiri sawasawa na wewe pia unapata mawazo mazuri mapya.

“Kama hakuna ubunifu maana yake hakuna maendeleo na huwezi kwenda popote, kwahiyo ubunifu ndio jambo linalokaa katikati ya maendeleo kwahiyo niwapongeze sana SUA kwa kuandaa siku hii na kusaidia shughuli za ubunifu ambazo mwisho wa siku bunifu hizi zitakwenda kusaidia taifa letu kupiga hatua za kimaendeleo” alisema Mhe.Wakili Msando.

Mheshimiwa Msando amewataka wabunifu wote nchini kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa changamoto za msingi kabisa kwenye jamii zinazowazunguka badala ya kufikiria kutatua matatizo makubwa pekee na kujikuta zipo changamoto ndogondogo nyingi ambazo wangeweza zitatua na kuifanya jamii kuishi vyema.



Profesa Amandus Muhairwa

Naye mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Utawala na Fedha) Profesa Amandus Muhairwa amesema Chuo Kimeandaa maonesho hayo ya ubunifu kama sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kuendeleza na kuimarisha teknoloja na maarifa asilia ya ndani ili yaweze kuchangia katika uchumi wa nchi lakini pia kuhamasisha na kukuza ubunifu na uvumbuzi kupitia sayansi na teknolojia nchini.

“Siku hii ni maandalizi ya Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu nchini yaani MAKISATU kwa mwa 2022, ambayo huwa yanaandaliwa na wizara ya Elimu sayansi na teknolojia ili kukuza ubunifu wa wazalendo nchini” alieleza Prof. Muhairwa.

Ameongeza kuwa matokeo tarajiwa ya siku hiyo ni kukua kwa hamasa ya ubunifu na kuchochea matumizi ya sayansi na teknolojia katika shughuli za kiuchumi na kijamii ili kufikia hatua ya ubiasharishaji kuchochea ugunduzi wa teknolojia na bidhaa mbalimbali.



Dkt. Doreen Ndossi

Akieleza chimbuko la Maonesho hayo, Mratibu wa Ubunifu na ushauri wa kitaalamu kutoka SUA Dkt. Doreen Ndossi ameeleza ni kuibua na kukuza ubunifu ili kuisaidia serikali katika sekta ya ubunifu hapa nchini.

“Maonesho haya ni sehemu ya maandalizi ya wiki ya kitaifa ya Ubunifu ambayo inatoa fursa kwa Wabunifu,Watunga sera,Wadhamini,Watafiti na wadau wote wa ubunifu nchini kuonesha kazi zao lakini pia kujifunza kwa wengine na kuunda ushirikiano baina yao kwenye sekta mbalimbali ili kuongeza kasi ya kitaifa kwenye matumizi ya teknolojia na ubunifu” alifafanua Dkt. Ndossi

Katika tukio hilo kulifanyika mawasilisho ya tafiti za kisanyansi, mdahalo pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali za ubunifu kutoka SUA na kwa wadau wengine ambapo lengo la maonesho hayo ni kuchangia juhudi na maendeleo ya kiuchumi.

Kauli mbiu ya tukio hilo ilikuwa ni “Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu”.



Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na Ushauri wa kitaalamu Prof. Esron Karimuribo akitoa neno la ukaribisho kwa wageni na washiriki











Habari na Picha: Calvin Gwabara - SUAMEDIA

 

Share this page