Mkuu wa Mkoa wa Lindi aipongeza SUA kwa kusaidia vijana kwenye fani za Kilimo

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainabu Telack amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kazi nzuri wanazofanya kwa kuandaa vijana na kuwapa elimu inayowawezesha kufanya ubunifu wa vitu mbalimbali pamoja na Kilimo ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

SUA

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainabu Telack (Wapili kulia) akiteta jambo na Waoneshaji katika banda la SUA

Pongezi hizo amezitoa Siku ya Alhamisi tarehe 12 Mei 2022 wakati alipotembelea Banda la SUA kwenye maonesho ya  tano ya Mifuko na Program za kuwezesha Wananchi kiuchumi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kuanzia tarehe 8 hadi 14 Mei 2022.

“Kama ikitokea watu wanasema kilimo ni fursa na vijana wakakubali kuingia kwenye kilimo haya maneno tunayosikia hakuna ajira yangekuwa yamekwisha kabisa hivyo niwaombe SUA kuendelea na jitihada hizi kubwa za kutoa elimu bora kupitia wataalamu wake” amesema Mhe.Telack

Mkuu wa mkoa alitolea mfano wa zao la korosho mkoani Lindi kwa kufafanua kwamba korosho kilo 5 zilizobanguliwa zinatoa kilo 1 ambayo huuzwa kwa shilingi elfu 20,000 mpaka 25,000, Hivyo ukiwa na hekari 3 za korosho tayari wewe ni mwajiri kwahiyo vijana waache kuangalia kilimo kama sio fursa na waanze kutumia taaluma zao kujikwamua kiuchumi. 

Mhe.Telack amekitaka Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine kuendelea kutoa elimu kwa Wanafunzi na Wananchi ili kuwasaidia kupata ujuzi zaidi na kuweza kuwasaidia vijana wengi Zaidi kujikwamua kiuchumi kwa kufanya  kilimo  biashara. 

Juditha Bernad kutoka Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu Cha Kilimo Cha Sokoine (SUGECO) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa alipotembelea banda la SUA

Kwa upande wake Juditha Bernad kutoka Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUGECO) ulioanzishwa mwaka 2011, ambao unasaidia vijana kuweza kujiari na kuajiri wengine amesema SUGECO iligundua kwamba vijana wengi wanaosoma masomo ya kilimo wanapomaliza hupata changamoto ya ajira, hivyo ushirika huu unanufaisha vijana kuweza kutumia taaluma zao kwa kujiajiri wenyewe.

Ameeleza namna wanavyonufaika kwa kufanyia kazi yale waliyojifunza kwa kutengeneza vitu vyenye ubora kupitia mazao mbalimbali yatokanayo na kilimo na hivyo kujikwamua kiuchumi. 

Ameainisha kuwa SEGECO kama ushirika unasaidia vijana hususani wale wanaosoma masomo ya kilimo kuweza kujiamini na kubadili mitizamo yao kwa kuchukulia masomo ya kilimo kama taaluma nyingine kwa kuwafundisha vijana waweze kuona kilimo kama fursa zingine. 

“Zipo program nyingi zinazofanyika kupitia wadau mbalimbali pamoja na Serikali kuweza kufundisha vijana kujihusisha na maswala ya kilimo biashara” alisema Juditha.



Athumani Sadala kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya mlaji - SUA akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Lindi vifaa mbalimbali ambavyo wananfunzi katika idara hiyo wanabuni na kuzalisha

Naye Mwakilishi kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya mlaji  SUA Athumani Sadala alieleza namna ambavyo wanatumia mabaki ya vitu visivyotumika kutengenezea bidhaa tofauti tofauti kama vile mapipa yasiyotumika kwa kuyakata na kutengenezea makochi, Matairi mabovu ya Baiskeli, bajaji na Pikipiki kutengeneza urembo.



Muonekano wa Banda la SUA kwene maonesho hayo kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro

Maonesho hayo ya tano yamehusisha mifuko ya uwezeshaji, Taasisi za fedha, Taasisi za serikali, Taasisi binafsi, Mashirika ya Umma na yasiyo ya umma, mashirika ya kimataifa na wajasiriamali.

Habari na Picha: Calvin Gwabara - SUAMEDIA

Share this page