Matokeo ya utafiti wa maji yaliyopo chini ya ardhi katika jiji la Dodoma

Matokeo ya Utafiti yanaonyesha kuwa shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo ya dakio la bonde la maji yaliyopo chini ya ardhi la makutupola ambalo ndio chanzo kikuu cha maji cha Jiji la Dodoma zinauwezekano mkubwa wa kuathiri uwepo wa chanzo hicho cha maji endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa kulinda chanzo hicho.

GROFUTURES

Picha ya pamoja ya Mgeni rasmi, Watafiti pamoja na wadau wengine kutoka sekta mbalimbali walioshiriki katika warsha hiyo ya kutoa matokeo ya utafiti huo

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mtafiti kutoka katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Profesa Japhet Kashaigili katika warsha ya kuwasilisha matokeo ya Utafiti uliokuwa una angalia namna ya kutumia maji yaliyopo chini ya ardhi kuondoa umasikini na uhaba wa maji katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara mbele ya wadau wa chanzo hicho cha maji uliofanywa na Watafiti wa SUA kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cardiff na Chuo Kikuu cha Jiji la London vyote vya nchini Uingereza.

Prof. Kashaigili amesema kuwa bila kukaa kwa pamoja kujadiliana kuangalia namna bora za kulinda eneo hilo sasa chini ya mpango wa upangaji wa Makazi, athari yake itakuwa kubwa huko baadae.

“Kuna haja ya kuyaangalia haya mapema ikiwezekana bonde hili litangazwe lote kwenye Gazeti la Serikali kuwa sehemu ya hifadhi ya bonde na liangaliwe kwa upekee wake ili kuzuia shughuli za kibinadamu ambazo zinaweza zikaathiri eneo lile kutokana na umuhimu wake kwakuwa karibuni zaidi ya  asilimia 90 za maji ya mji huu wa Doodoma yanatoka pale ”, ameeleza Profesa Kashaigili.

Aidha Prof. Kashaigili ameongeza kuwa kwakuwa mvua kwa miaka ya karibuni hazijaweza kufikia zile za El nino basi zinaweza tumika mbinu zingine ambazo zimetumiwa na nchi zingine duniani za kuchimba visima na kuruhusu maji kujaa kwenye eneo hilo na kuyaacha yaingie kwenye mwamba huo ardhini na kisha kuweza kuyatumia kupelekwa kwenye maeneo mengi zaidi ya jiji la Dodoma.

“Inawezekana haya maji tukayatathimini ubora wake lakini tukayaruhusu yakakaa juu ya ardhi kwakuweka mazuio mbalimbali ili yaweze kunywea kuingia ardhini jambo ambalo nchi mbalimbali zimefanya hivyo na zimefanikiwa kuondoka na adha zilizopo za upatikanaji wa maji”, alifafanua Profesa  Kashaigili.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Profesa Japhet Kashaigili akifafanua jambo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt George Lugomela ameeleza kuwa kwa siku jiji la Dodoma linahitaji maji yenye lita za ujazo 133,845 lakini upatikanaji wake ni lita za ujazo 66,600 kwa siku ambayo ni kama nusu ya mahitaji na hii ni kutoka na ongezeko la watu katika jiji hilo.

“Serikali tayari imeweka mikakati Madhubuti katika kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa ikiwemo kujenga bwawa la FAKWA lakini mkakati wa haraka ni kuchukua maji lita za ujazo 100,000 kwa siku kutoka bwawa la Mtera  ambazo ukichanganya na zile 66,600 za sasa unapata lita za ujazo 166,600 ambazo zitakuwa na uwezo wa kukidhi kabisa mahitaji ya Jiji lote la Dodoma” alifafanua Dkt. Lugomela.

Hivyo amesema kuwa matokeo ya Utafiti huo ni muhimu sana na yatatumiwa na Wizara katika kuwezesha kutazama namna ambavyo itawezekana kutatua changamoto hiyo ya maji kupitia chanzo cha Makutupola tofauti na ilivyo hivi sasa.

Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji Dkt George Lugomela akitoa neno wakati akifungua warsha hiyo ya siku moja ya kupokea matokeoa ya utafiti wa mradi wa GroFutures Jijini Dodoma

Naye Mtafiti Mkuu wa mradi huo  Profesa Richard Taylor kutoka katika Chuo Kikuu cha jiji la London nchini Uingereza amesema kuwa mradi huo unatekelezwa katika nchi tatu ambazo ni Tanzania, Nigeria na Ethiopia pamoja na malengo mengine lakini pia ulilenga kuangalia namna maji yaliyo chini ya ardhi yanavyoweza kuchangia katika kuondoa umasikini.

Ameeleza kuwa maji ya chini ya ardhi hayawekewi mkazo sana kama ilivyo kwa maji ya juu ya ardhi hivyo ameishauri serikali kuwekeza katika maji yanayopatikana chini ya ardhi kwakuwa kuna maji mengi kuliko haya tunayoyaona juu ya ardhi yanayopita kwenye mito na maziwa.

“Naishauri Serikali kuwekeza nguvu, muda pamoja na kuwajengea uwezo watu wake katika kutambua rasilimali hii ya maji yaliyopo chini ya ardhi kwani itasaidia katika kukabiliana hata na mabadiliko ya tabia nchi na kuchangia katika matumizi mbalimbali kama vile Kilimo,Viwanda na matumizi ya nyumbani ”, alisema Profesa Taylor.

Mtafiti Mkuu wa Mradi huo  Profesa Richard Taylor wa Chuo Kikuu cha jiji la London nchini Uingereza akichangia kwenye uwasilishaji wa matoke hayo

Kwa upande wake mmoja ya wakulima ambao wamepata nafasi ya kuhudhuria Warsha hiyo kwa niaba ya wakulima wengine Dkt. Huruma Msuya ameishauri Serikali kutenga maeneo maalumu kwaajili ya misitu, kilimo cha mbogamboga na matunda kwaajili ya kulisha miji  jambo litakalosaidia mji kuwa na sehemu ya kupumulia. 

“Tusifanye makosa kama yaliyofanyika kwenye Jiji la Dar Es Salaam ambapo mji umekuwa kutoka Kariakoo mpaka Kibaha bila kuwa na maeneo yenye mashamba na Misitu, mji usikue tu kuwe na miji midogo midogo pembeni ya mji mkubwa ambayo nayo itakuwa imeendelea, itakuwa inapata maji hukohuku kupunguza hali ya upatikanaji wa maji kutoka upande mmoja”, alisema Dkt Msuya. 

Matokeo yaliyowasilishwa  ni ya Utafiti uliofanyika kwa miaka mitano kupitia mradi wa GroFutures ulioanzishwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Chuo cha Cardiff pamoja na  Chuo Kikuu cha jiji la London vyote vya nchini Uingereza .

Imeandikwa na: Amina Hezron na Calvin Gwabara - SUAMEDIA
 

Share this page