Majani ya JUNCAO kuwa suluhisho la malisho ya mifugo

Wafugaji nchini Tanzania wametakiwa kuanza kulima majani aina ya JUNCAO yanayozalishwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kutokana na majani hayo kuonekana kuwa na faida nyingi kwa mifugo na uwezo wake wa kukua haraka na kuvumilia ukame na hivyo kupunguza changamoto za malisho wakati wa kiangazi na kumaliza migogogo ya wakulima na Wafugaji.

SUA

Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa Nyasi za JUNCAO kutoka SUA, Dkt. Elly Ligate akikabidhi miche kwa mmoja wa wafugaji

Wito huo umetolewa siku ya Alhamisi, Juni 23, 2022 na Mkuu wa Idara ya Sayansi za Viumbe Hai na Mtafiti wa Malisho Dkt Beda Mwang’onde wakati wakikabidhi vipando vya miche ya nyasi za malisho hayo aina ya JUNCAO kwa wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Lugala ili kukabiliana na changamoto ya malisho na kuacha kulisha kwenye mashamba ya wakulima na yale ya Chuo.

 “Aina hizi za nyasi sio malisho tu, bali yanatumika pia kuzalishia Uyoga. Tumeandaa kitalu maalumu kwaajili ya kuzalishia Uyoga kwakutumia haya majani tuone Uyoga utakuwa wa aina gani lakini lengo letu kubwa ni kuzalisha Uyoga dawa pamoja na kupata mbegu ili kuweza kutunza baadhi ya maeneo ya Chuo yanayoathiriwa na mmomonyoko wa udongo”, alisema Dkt Beda.

Mkuu wa Idara ya Sayansi za Viumbe Hai na Mtafiti wa Malisho Dkt Beda Mwang’onde akizungumza kuhusiana na upatikanaji wa nyasi hizo SUA 

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa Nyasi za Malisho hayo kutoka SUA, Dkt. Elly Ligate ameelezea matumizi mengine ya nyasi hizo ni pamoja na malisho kwa samaki, kuhifadhi udongo na kutunza vyanzo vya maji ambapo nchini China hutumika kuzalisha mbao na karatasi na nyasi hizo zinasaidia pia kufyonza hewa ukaa.

Amesema utafiti wa kuboresha Nyasi hizo umefanyika nchini China kwa zaidi ya miaka 20 na kugundulika kuwa na virutubisho vingi muhimu kwa mifugo na kuzifanya zipendwe sana na Wanyama ikiwemo,Ng’ombe,Mbuzi,Kondoo na mifugo mingine kama vile kuku na Bata.

“Nyasi hizi tayari tumeshazisambaza katika mashamba mbalimbali likiwemo la Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye shamba lake la mifugo Msoga na maeneo mengine nchini hivyo wakulima na wafugaji wajitokeze kuchukua mbegu hizo na kuzipanda ili kukabiliana na changamoto ya malisho”, alisema Dkt Ligate. 

Mmoja ya wafugaji Sanga Mkulago akizungumza jambo na Dkt Ligate kuhusiana na malisho

Akizungumza mmoja ya wafugaji waliopata mbegu hiyo Sanga Mkulago amewashukuru wataalamu wa SUA kwakuwapatia elimu pamoja na mbegu hizo zitakazokuwa mkombozi kwa mifugo yao na amewataka wafugaji wengine kuhakikisha wanasikiliza maelekezo ya wataalamu na kulima nyasi hizo.

“Tumepata mbegu na tutaiendeleza pamoja kwakushirikiana na wataalamu tunateseka sana katika kipindi cha kiangazi lakini kwasasa kwakupitia haya majani naamini yatatusaidia kupata maziwa yakutosha”, alisema Sanga.

Majani hayo aina ya JUNCAO kutoka Nchini China kitalu chake kipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo yanagawiwa kwa Wakulima na wafugaji mbalimbali nchini na yanaendelea kufanyiwa utafiti zaidi kwa mazingira ya Tanzania.

Dkt Ligate akionyesha namna ya nyasi za malisho aina ya JUNCAO zilivyo



Dkt Ligate akitoa maelezo kwa wakulima na wafugaji namna ya upandaji wa miche ya nyasi hizo

Imeandikwa na Amina Hezron - SUAMEDIA
 

Share this page