Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia kitengo cha SUA Innovation Hub, kwa kushirikiana na kampuni ya AQUILA EYES GROUP (AEG) ya Morogoro nchini Tanzania kwa udhamini wa “The Belt and Road Geospatial Information Training Center (BRGTC)” wamefanikiwa kuendesha mafunzo ya siku tatu ya kimataifa ya matumizi ya mifumo ya taarifa za kigeographia (GEOSPATIAL INFORMATION SCIENCE) katika kutambua na kutatua changamoto mbalimbali za upatikanaji wa taarifa na matumizi yake katika sekta mbalimbali nchini.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa shahada za juu, utafiti uhawilishaji wa teknolojia na ushauri wa kitaalamu Dkt.Aquilina Mwanri amepongeza jitihada kubwa zilizofanywa na wadau hao na kufikia hatua ya kuendesha mafunzo hayo ya kwanza nchini, katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro na kuomba SUA iwe kitovu/kituo ambacho kitasaidia kutoa mafunzo haya kwa wadau mbalimbali katika matumizi ya teknolojia hiyo kwa kushirikiana na mdau mwenza (AQUILA EYES GROUP).
“Nimefurahishwa kusikia kuwa kituo kinakuwa na malengo mbalimbali ambayo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa taaluma mbalimbali zinazohusu uchunguzi na maswala ya mifumo ya sayansi ya kijografia (GIS) na ufafanuzi wa picha za anga (satellite images) kwa wanataaluma, taasisi na sekta binafsi kwa lengo la kuwaunganisha na kuhakikisha ushirikiano katika maswala ya Taarifa za jongrafia (GIS) lakini pia kubwa zaidi ni kutambua wadau katika matumizi ya teknolojia hii ikiwemo wanafunzi, taasisi binafasi na zile za kiserikali” Alisema Dkt. Mwanri.
Ameongeza kutokana na umuhimu wa teknolojia hiyo ameomba waandaaji wa mafunzo hayo kuona sababu ya kuendesha mafunzo ya mara kwa mara nchini ili kuweza kuwafikia wadau wengi zaidi katika matumizi ya teknolojia hiyo ili iweze kurahisisha kazi zao na kuchochea uchumi wa taifa hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi hawaifahamu na hawatambui namna inavyoweza kurahisisha kazi zao za kila siku kwenye taasisi zao.
Dkt. Mwanri amesema anatambua ukuaji mkubwa katika teknolojia za kijografia lakini bado nchini tunazo changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na utaalamu, mbinu na matumizi ya teknolojia kuwa machache, hivyo ni wakati sasa vijana walio kwenye fani hizo kuchangamka na kutafuta elimu zaidi na za kisasa kwenye maeneo hayo nchini.
“Mafunzo haya ya Teknolojia hii ya mfumo wa taarifa za kijiografia (GIS) na ufafanuzi wa picha za anga (Remote Sensing) nchini ni muhimu sana katika kuiunganisha Serikali na wadau lakini pia inagusa maswala ya Afya, majanga kama mafuriko, tetemeko la ardhi, moto, uharibifu wa misitu, na mambo mengine mengi hivyo ni muhimu kuendesha mafunzo haya mara kwa mara ambayo yatawezesha kuongeza ufanisi katika kupata taarifa mbalimbali ambazo zipo kwenye mfumo huo kwa matumizi mbalimbali ya kimaendeleo” Aliongeza Dkt. Mwanri.
Nae kwa upande wake Dkt. Doreen Ndossi ambaye ni Mratibu wa uhawilishaji wa teknolojia na ushauri wa kitaalamu kutoka SUA amesema ni fursa kubwa ambayo Chuo imeipata kupitia mkataba huo wa ushirikiano na wadau hao ambao umefanikisha mafunzo hayo ambayo yanakwenda kusaidia kujenga uelewa kwa wadau juu ya matumizi ya teknolojia hiyo ya kisasa.
‘’Sisi kama Kurugenzi tunaona uwepo wa teknolojia hiyo utasaidia sana katika kutoa taarifa mbalimbali muhimu za kazi tunazofanya Chuoni kwa wadau wetu mbalimbali na kufikia jamii kubwa zaidi na ndio msingi hasa wa mkataba wa makubaliano (MoU) tuliyosaini ili kufanya kazi nao kwa pamoja na kwa ukaribu kwa manufaa mapana ya Chuo na Taifa letu” Alibainisha Dkt. Ndosi.
Awali Mratibu wa mafunzo hayo nchini Dkt. Neema Sumari alisema kuwa wanafanya mafunzo hayo kwa kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali wa sekta binafsi na za kiserikali ili kuweza kuwafundisha namna ya kutumia mfumo huo wa kisasa ili waweze kwenda kuutumia na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
“Kwa kutumia mfumo huo utasaidia kupunguza gharama na muda katika kupata taarifa mbalimbali za kila sekta kulingana na mahitaji yao na kupitia mkataba wa makubaliano (MoU) kati ya SUA na iSpatial wanaweza kupata taarifa na elimu muhimu wanazohitaji kwa urahisi tofauti na sasa” Alibainisha Dkt. Sumari.
Dkt. Sumari alisema kwa mwaka huu ushirikiano huo umefanyika katika nchi mbili za Afrika ikiwemo Afrika ya kusini na Tanzania, na tayari mafunzo kwenye nchi hizo yamefanyika. Ambapo kila nchi imechagua mada kuu ya mafunzo, kwa kulingana na mahitaji ya taasisi mbali mbali kwa wakati huo.
Kufungwa kwa Mafunzo
Wakati wa kufunga mafunzo hayo, mkurugenzi wa kurugenzi ya shahda za juu, Utafiti, Uhawilishaji wa teknolojia na ushauri wa Kitaalamu Prof. Esron Karimuribo alipongeza ushiriki mzuri wa wadau mbalimbali kwenye mafunzo hayo na kusema kuwa SUA itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kuwezesha mafunzo mengine ya aina hiyo yaweze kufanyika tena chuoni hapo kulingana na mahitaji ili yaweze kuwanufaisha watu wengi zaidi na taasisi zao.
‘’Nimefurahishwa na mada mbalimbali zilizotolewa kwenye mafunzo haya lakini kubwa zaidi ni kitendo cha kuwakutanisha wataalamu kutoka katika taaluma mbalimbali na kuzungumzia maswala ya afya,majanga kama mafuriko,tetemeko,Moto uharibifu wa misitu na mengine mengi yanayozunguka jamii na nchi yetu’’ Alibainisha Prof. Karimuribo.
Aidha amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia katika kuanzisha mashirikiano na wadau muhimu kama vile maafisa wa serikali, asasi za kiraia, watumishi wa serikali katika ngazi za serikali za mitaa na ngazi ya kitaifa pamoja na sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kwa maswala ya kiuchumi na maendeleo ya jamii.
Amewataka washiriki hao kwenda kuyatumia mafunzo hayo vizuri na kuwafundisha wenguine kwenye taasisi wanazotoka ili yaweze kusaidia kurahisisha utendaji wa kazi zao.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo nchini Dkt. Neema Sumari amesema wao kama waandaaji wapo tayari kuendelea kutoa mafunzo kwenye taasisi na mashirika wanayotoka kulingana na mahitaji yao pale itakapohitajika.
‘’Huu ni mwanzo mzuri kwakuwa ndio mafunzo yetu ya kwanza kufanyika nchini lakini niwaombe mfikishe salamu hizo kwenye maeneo mnayotoka na kwa viongozi wa taasisi zenu na ikiwezekana nanyi muweke kuingia mikataba ya makubaliano na BRGTC ili mnufaike moja kwa moja kwakuwa nafasi hiyo ipo’’ Alieleza Dkt. Sumari.
Pia amewataka kuchangamkia fursa zinazotolewa na chuo kikuu cha Wahung cha nchini China za kwenda kusoma kwakuwa kinatofa nafasi za ufadhili wa masomo kwa wanaotaka kusomea maswala ya teknolojia hiyo kwakuwa ni chuo kilichobobea katika maswala hayo duniani.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wengine, Dkt. Chris Migomba ambaye ni mtafiti na mhadhiri kutoka SUA amesema amejifunza mambo mengi sana hasa namna ya kupata taarifa mbalimbali ambazo sio rahisi kuzipata kwa njia ya kawaida.
‘’Mimi ni mtafiti na kwakweli tunapata tabui sana kwenye kupata taarifa na data mbalimbali kwenye tafiti zetu hata unapokwenda NBS pia kuna changamoto zake lakini nimeona kwa kutumia teknolojia hii kunarahisha sana kupata taarifa mbalimbali muhimu katika tafiti na hivyo kurahisisha kazi’’ Alieleza Dkt. Chris.
Amewaasa vija kuchangamkia fursa za masomo zinazotolewa na chuo hicho cha china na kuwataka kujikita zaidi kwenye matumizi ya teknolojia hiyo ambayo inakua kwa kasi na yenye mchango mkubwa katika kufanya tafiti mbalimbali.
Mafunzo hayo ya kwanza nchini ambayo ni ya siku tatu, yamefanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 mwezi wa 12 mwaka 2021 na kuwakutanisha wadau kutoka mashirika na taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali kama vile TANECO,MORUWASA,Manispaa ya Morogoro, TARURA,ARIMO, wanafunzi, SUA, Mzumbe na wengine yamefadhiliwa na BRGTC na kuandaliwa na SUA pamoja na kampuni ya AQUILA EYES GROUP kwa uratibu wa kitengo cha SUA Innovation Hub