Jaji Warioba aahidi kusaidia utatuzi wa changamoto za kilimo

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mhe. Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba ameahidi kufanya kazi bega kwa bega na wanajumuiya wa chou ili kuhakikisha chuo kinapiga hatua na kuendele kutatua changamoto katika kilimo hususani katika mazao yanayozalisha mafuta ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa mafuta nchini

SUA

Mhe. Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha utoaji taarifa ya utekelezaji wa mafanikio ya Chuo kwa kipindi cha miaka mitano 2017 - 2022 kilichofanyika katika ukumbi wa Multipurpose, Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine siku ya Alhamisi tarehe 26 Mei, 2022. 

Aidha Jaji Warioba ametoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya sita kwa kufanya kazi bega kwa bega na Chuo licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo uviko19 na kupongeza utendaji kazi shirikishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda pamoja na wafanyakazi wa jumuiya ya SUA kwa ujumla. 

“Mafanikio yaliyopatikana ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali chuoni hapa kwa kipindi cha miaka mitano ni kutokana na bidii pamoja na ushirikiano baina ya uongozi na wafanyakazi hivyo basi malengo tarajiwa yanategemea ushirikiano huohuo kwa miaka mingine mitano ijayo”. Amesema Jaji Warioba. 

Awali Mhe. Jaji Warioba alitembelea baadhi ya vitengo mbalimbali vya chuo nakujionea kazi mbalimbali zinazofanyika ikiwemo idara ya sayansi ya uhandisi kilimo, Maabara  Mtambuka na kituo atamizi cha mafunzo ya Kilimo biashara ambapo aliweza kuona vijana wanavyoweza kufanya Kilimo cha kisasa na kupata faida kubwa. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu Mhe. James Mdoe ameupongeza uongozi wa chuo kwa kazi kubwa ambayo wameifanya na kuwataka kufanya kazi kwa nguvu zaidi kutokana na kukua kwa teknolojia na kuhakikisha wanapata maarifa ya kutosha kinadharia na vitendo.

Ameongeza kuwa katika malengo waliyoweka kwa kipindi cha miaka mitano mingine wanapaswa kuwa na mikakati thabiti katika kuhakikisha wanaandaa mazingira rafiki ambayo yanaweza kukabiliana na idadi ya wanafunzi inayoongezeka kila mwaka na zaidi katika ufundishaji kwa vitendo ili kutoa wataalam waliobobea kwa njia ya nadharia na vitendo.

Profesa Raphaeli Chibunda

Naye makamu mkuu wa chuo, Profesa Raphaeli Chibunda aliainisha ushiriki mzuri wa chuo katika kufanya Tafiti, ambapo chuo kimekuwa kikishirikiana na wadau wa maendeleo katika kufanya Tafiti hizo, ambapo Tafiti nyingi hufanyika mashambani na wakulima wanashirikishwa moja kwa moja ili kuwasaidia kujifunza mbinu bora za Kilimo ambazo zitawawezesha kuboresha uzalishaji na kupunguza umaskini.










Share this page