Takribani zaidi ya wananchi 200 katika kata za Magulilwa, Mgama pamoja na Mbalamaziwa zilizopo wilaya ya Iringa vijijini na Mufindi mkoani Iringa zimenufaika na mafunzo yanayohusu Matumizi ya Bundi katika kudhibiti Viumbe hai waharibifu wa mazao shambani hususani panya.
Mafunzo hayo yametolewa na Watafiti wa Mradi wa Mtazamo wa Wakulima kuhusu kutumia Bundi kukabiliana na Viumbe visumbufu katika mazao kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Dkt. Nicolaus Mwalukasa Mtafiti Mkuu katika Mradi huo amesema tafiti zinaonesha kwamba moja kati ya Viumbe visumbufu katika mazao ni Panya ambao huwa wanaharibu mazao ya nafaka kwa 5% - 15% kwa mwaka na wakulima wamekuwa wakitumia kemikali zaidi kukabiliana na viumbe hao.
Amesema wamefanya Tafiti na kuja na mbinu mbadala na rafiki kwa mazigira yenye kuweza kukabiliana na Panya kwa kutumia Bundi na ieleweke kwamba Bundi ni ndege ambaye ni rafiki kwa maana kwamba ana uwezo wa kusaidia kula viumbe kama Panya ambavyo ni visumbufu vya mazao ya wananchi wengi.
“Katika kukabiliana na visumbufu vya mazao ambao ni panya tumewafundisha wakulima namna gani wanaweza wakafanya ili kuwezesha Bundi kukabiliana na panya hao ikiwemo kuwatengenezea viota na kuviweka katika mashamba ambapo wakati wa mchana Bundi watakaaa katika vile viota na usiku wataweza kutoka na kwenda kukabiliana na Panya”, amesema Dkt. Mwalukasa.
Wananchi wa kijiji cha Mgama kata ya Mgama wilayani Iringa vijijini wakifuatilia kwa umakini na kusikiliza mafunzo yanayohusu kutumia Bundi katika kukabiliana na viumbe visumbufu katika mazao
Kwa upade wake Bi. Anna Kimaro ambaye pia ni Mtafiti katika Mradi huo amesema wananchi wanatakiwa kuachana na fikra potofu za kufikiria kwamba Bundi anatumika katika masuala ya kishirikina badala yake watambue kuwa anaweza kutumika katika kudhibiti viharibifu vya mazao.
“Watu wamekuwa na dhana ya kwamba Bundi anatumika tu kwenye ushirikina na kusahau kuwa bundi ni ndege tu kama walivyo ndege wengine na milio yake ndio inawatisha watu zaidi wakati ni milio tu kama wanavyolia ndige wengine au wanyama, hivyo basi elimu hii itamsaidia sana mkulima na kujua kwamba Bundi ana faida kubwa sana akiwa kama mlinzi wa viumbe waharibifu wa mazao”, amesema Bi. Kimaro
Naye Denis Chaula ambaye ni mshiriki katika mafunzo hayo kutoka kata ya Magulilwa amesema elimu aliyoipata imemsaidia kujua kuwa Bundi ni zaidi ya kile alichokuwa anakiamini na kuwa wana faida kubwa katika kulinda mazao dhidi ya viumbe sumbufu kama panya.
Kwa upande wake Safia Madenge ambaye pia ni mshiriki kutoka katika kata hiyo ya Magulilwa amesema elimu hiyo imemsaidia sana kumuelewa bundi na kazi zake na ameiomba serikali kuendelea kutoa elimu zaidi ili kuwafungua macho wakulima waweze kuondokana na hasara wanazozipata kutoka kwa viumbe sumbufu.
Ndugu Denis Chaula (Mchungaji) aliyesimama akiuliza swali katika mafunzo yanayohusu matumizi ya Bundi katika kuthibiti viumbe visumbufu katika kata ya Magulilwa wilayani Iringa vijijini
Mmoja kati ya wakulima kutoka kata ya Mbalamaziwa (kushoto) akimuelekeza Dkt Nicolaus Mwalukasa maeneo mazuri kwa kuweka viota ambavyo watakuwa wanaishi bundi katika kukabiliana na wadudu wasumbufu katika mashamba wilayani Mufindi mkoani Iringa
Dkt Nicolaus Mwalukasa akiwaelekeza jinsi ya kuweka kiota katika Mashamba