Agenda za Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji 2020/ 2025 zazinduliwa SUA

Siku ya Jumamosi tarehe 16 Novemba 2019, Wizara ya mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) walizindua agenda za kitaifa za utafiti wa masuala ya Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji viumbe maji kwa mwaka 2020/2025, tukio ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Nelson Mandela Freedom Square, Chuo Kikuu cha Sokoine  Kampasi ya Solomon Mahlangu. 

uzinduzi wa Agenda za kitaifa za mifugo na uvuvi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Agenda za Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025, wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mh. Loata Ole Sanare, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Abdalah Ulega na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Profesa Raphael Chibunda 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina (MB) alizindua agenda hizo na kueleza malengo yake ikiwa ni pamoja na (i) kuzifungua tafiti zilizofanyika miaka ya nyuma na kuzifikisha kwa watumiaji (ii) kuweka utaratibu wa kutambua, kuorodhesha na kutumia tafiti zinazofanywa na wanafunzi wa shahada za uzamili (iii) kuweka kanuni zinazotoa muongozo wa utekelezaji wa agenda na kuhakikisha watafiti wanatekeleza wajibu wao na (iv) kuweka utaratibu wa kuwaunganisha watafiti wa mifugo na uvuvi. Agenda hizi pia zinalenga kuweka msingi wa kusimamia watafiti kufuatana na mahitaji ya soko na mambo muhimu kitaifa pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani kwenye bidhaa za mifugo na uvuvi. 
 

Mpina
Mh. Luhaga Mpina (MB)

Katika tukio hilo, waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Joelson Mpina (MB) alieleza pia kuwa kwa muda mfupi tangu Serikali ya awamu ya  tano chini ya Rais John Pombe  Magufuli iingie madarakani imefanikiwa  kuongeza kiwango cha ukusanyaji  mapato ya sekta ya Mifugo na Uvuvi  kutoka  billion 21 hadi shilingi bilioni 72. Amesema  kuwa kwa mwaka ujao wa fedha sekta ya Mifugo na Uvuvi  inatarajia kuongeza mapato zaidi na kufikia  kiasi cha shilingi bilioni 80.

Amesema  licha ya ongezeko  la mapato, Serikali kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kudhibiti uingizwaji holela wa zao la Mifugo na Uvuvi  nchini kitendo kilichokuwa kinapelekea  Wafugaji na Wavuvi wa ndani ya nchi  kukosa  soko na ushindani kukosekana mana wanafuga lakini hawapati soko.

“Nataka niwaambie ya kwamba hadi leo uagizaji wa samaki kutoka nje umeshuka kwa asilimia 67 na mwaka huu tunaoenda hata asilimia 2 haijafika ya kuagiza samaki kutoka nje ya nchi,  Hiyo ina maana bilioni 56 zilizokuwa zikitumika na watanzania kuagiza samaki kutoka nje zitatumika hapahapa nchini,” amesema Waziri Mpina.

Wakati huohuo  amesema kuwa ajira zimeongezeka kutokana na ongezeko la viwanda ambalo pia limechochea uwekezaji katika sekta ya Mifugo na Uvuvi, Pia ameshukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwa wenyeji  wa uzinduzi huo huku akiongeza kuwa Chuo hicho ndio chimbuko kuu la Watafiti wengi wa sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini.

Mkuu wa Mkoa Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro

Awali akimkaribisha Waziri wa mifugo na uvuvi kuzungumza,  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Erasto Sanare amemshukuru Waziri Mpina kwa kuchagua mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji wa uzinduzi huo  na kuongeza kuwa hayati Mhe. Sokoine alikuwa  ni mfugaji hivyo kuchagua Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  SUA kufanyia uzinduzi huo ni kumuenzi kwa vitendo. Amesisitiza kuwa  mkoa wa Morogoro una wafugaji wengi  hivyo amefurahi kuona  uzinduzi huo  umefanyika mkoani  hapo kwani  tafiti zitasaidia kufuga kitaalam na kutatua migogoro iliyopo kati  ya wafugaji  na wakulima.
 

Chibunda

Prof. Raphael Chibunda

Naye Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Waziri Mpina kwa kuchagua SUA  kuwa sehemu ya uzinduzi huo na pia wanathamini mchango wa Wizara ya Mifugo na uvuvi na kuahidi kuwa sehemu ya utekelezaji wa agenda za utafiti huo.
 

Uzinduzi wa agenda za kitaifa za mifugo na uvuvi


Fuatilia kilichojiri kwenye tukio hilo kwa kupitia video ifuatayo kama ilivyoandaliwa na SUAMEDIA ...

 

 SOMA PIA:  NDAKI YA KILIMO YASHIRIKI UZINDUZI WA AGENDA ZA UTAFITI WA MIFUGO, UVUVI NA UKUZAJI WA VIUMBE MAJI

 

Share this page